Vyama vya Ford-K na ANC kuvunjwa kuunda chama kimoja
LEONARD ONYANGO na GAITANO PESSA
VIONGOZI kutoka eneo la Magharibi wamedokeza mpango wa kutaka kuvunjilia mbali vyama vya Amani National Congress (ANC) na Ford-Kenya ili kuunda chama kipya watakachotumia katika uchaguzi wa 2022.
Viongozi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Ford-Kenya, Eseli Simiyu, Naibu Kiongozi wa ANC Ayub Savula, mbunge wa Butere Tindi Mwale, mbunge wa Nambale Sakwa John Bunyasi na mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba walisema hatua hiyo inalenga kuunganisha jamii ya Waluhya.
Wanasiasa hao waliokuwa wakihutubia wanahabari jijini Nairobi walisema jamii ya Waluhya imechoka kutumiwa vibaya na wanasiasa kutoka nje na kisha kutelekezwa.
“Kwa muda mrefu jamii ya Waluhya imekuwa ikitumiwa na wanasiasa kutoka nje na kisha kututelekeza,” akasema Bw Eseli.
Mbunge huyo wa Tongaren alisema viongozi wote ambao sasa wako katika vyama vya ANC na Ford Kenya watajiunga na chama kipya kitakachokuwa na sura ya kitaifa.
Alisema baadhi ya wabunge waliochaguliwa kupitia vyama vya ODM na Jubilee katika ukanda wa Magharibi tayari wameunga mkono pendekezo la kutaka kubuniwa kwa chama kipya kitakachounganisha jamii ya Waluhya.
Tayari kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya wameanza mchakato wa kuunganisha Waluhya huku wakimshutumu kinara wa ODM Raila Odinga kwa kuhadaa na kusaliti jamii hiyo.
Adui wa Raila
Bw Wetang’ula amegeuka kuwa adui wa Bw Odinga tangu alipong’olewa kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wachache katika Seneti na nafasi hiyo kuchukuliwa na Seneta wa Siaya James Orengo.
Uhasama baina ya ODM na vyama vingine vilivyomo katika mwavuli wa NASA, ANC, Wiper na Ford-Kenya ulizuka baada ya Bw Odinga kutoroka vinara wenzake na kutangaza kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta.
“Jamii ya Waluhya imekuwa ikichukuliwa kama watu waliotengana, lakini tunataka kuonyesha kuwa tunaweza kuungana na kuzungumza kwa sauti moja. Tunaonya vikali wanasiasa ambao wamekuwa wakitugawanya,” akasema Bw Eseli.
Ikiwa vyama vya ANC na Ford Kenya vitavunjiliwa mbali inamaanisha kuwa huo utakuwa mwisho wa muungano wa NASA.
Walitoa kauli hiyo huku Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong’ akisema yuko tayari kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa muungano wa upinzani Raila Odinga kwa manufaa ya wakazi.
Kuzika tofauti
Viongozi hao wawili hasimu Februari waliamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kukubaliana kushirikiana ili kuleta utangamano nchini hasa baada ya kipindi kirefu cha siasa mwaka jana.
Bw Ojaamong ambaye alipongeza hatua ya wawili hao kushirikiana, alisema msimu wa siasa ulimalizika.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi wa maji wa Sh 30 milioni katika eneo bunge la Budalangi, Bw Ojaamong alitoa wito kwa Rais Kenyatta kutochagua viongozi walioshindwa uchaguzini kujaza nyadhifa muhimu.
“Iwapo mtu alitemwa na wananchi sioni haja ya rais kumpa wadhifa mwingine. Ni vyema rais awateue watu wengine wanaoweza kuwajibika ipasavyo,” akasema.
Kauli yake huenda iliwalenga wabunge wa zamani Paul Otuoma (Funyula), Ababu Namwamba (Budalangi), Mary Emaase (Teso Kusini), Arthur Odera (Teso Kaskazini) na Michael Onyura (Butula).
Baadhi ya wabunge hao waliapa kufanya kazi na chama tawala cha Jubilee. Tayari Bw Ababu aliteuliwa na Rais katika wizara ya maswala ya nje.