• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wagonjwa 400 wanufaika na matibabu ya bure

Wagonjwa 400 wanufaika na matibabu ya bure

Hospitali Kuu ya King Fahad mjini Lamu ambako matibabu ya bure yalifanyika. Picha/Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

WAGONJWA zaidi 400  kutoka maeneo mbalimbali ya Lamu wamenufaika na kambi ya matibabu ya bure iliyoandaliwa na serikali ya kaunti ya Lamu kwa ushirikiano na madaktari maalum wa upasuaji kutoka nchini Uhispania.

Matibabu hayo yaliyokuwa yakiendelea katika hospitali kuu ya King Fahad kwa wiki tatu mfululizo yalifikia ukingoni Alhamisi.

Akizungumza na Taifa Leo, Waziri wa Afya wa Lamu, Raphael Munyua, alisema mpango huo ulilenga hasa kuwasaidia wagonjwa ambao hawangeweza kukimu gharama ya matibabu kutokana na umaskini.

Alisema kaunti itaendelea kushirikiana na wahisani tofauti tofauti ili kuona kwamba wakazi wanapokea huduma bora za matibabu kote Lamu.

“Tunashukuru wahudumu maalum wa afya kutoka Uhispania. Tumeshirikiana vyema katika kufanikisha kambi hii ya bure ya matibabu. Zaidi ya wagonjwa 400 wa hapa Lamu wamepokea upasuaji na hata ushauri wa bure kutoka kwa madaktari wa uhispania na pia wa papa hapa nyumbani,” akasema Bw Munyua.

Kwa upande wake, Daktari Mkuu aliyeongoza madaktari wengine wa upasuaji kutoka uhispania, Daniel Casanova alieleza kufurahishwa kwake na ushirikiano uliokuwepo kati ya kaunti na timu yake ambao ulifanikisha shughuli hiyo.

Dkt Casanova alisema bado kuna haja ya hospitali za Lamu kuboreshewa miundomsingi itakayowezesha hospitali hizo kuhudumia wagonjwa wa upasuaji na huduma nyingine muhimu hospitalini King Fahad.

“Tumekamilisha shughuli ya matibabu ya bure na tunashukuru kaunti kwa usimamizi wake na ushirikiano uliowezesha sisi kufanikisha kambi hili la matibabu ya bure. Ninalosisitiza ni miundomsingi kuimarishwa hospitalini. Bado kuna upungufu wa vifaa vya kutekelezea matibabu mengi spesheli, ikiwemo upasuaji,” akasema Dkt Casanova.

Kwa upande wake, Dkt Mkuu wa Upasuaji katika hospitali ya King Fahad, Danson Makhanga, aliiomba kaunti kuongeza madaktari zaidi maalum eneo hilo ili kukimu idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji matibabu spesheli.

“Lamu iko na hospitali tatu kuu, ikiwemo King Fahad, Mpeketoni na Faza. Mimi pekee ndiye daktari maalum wa upasuaji. Itakuwa bora kwa kaunti kuajiri madaktari zaidi ili kusaidia kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa wenye uhitaji hapa Lamu,” akasema Dkt Makhanga.

You can share this post!

Watalii wafurika Lamu kusherehekea Pasaka

Shule zisizopaka mabasi yao rangi ya manjano kuona cha moto

adminleo