Mshukiwa asimulia walivyomtoa Padri kafara
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA iliamuru Ijumaa kwamba wanaume wawili wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya kasisi wa Kanisa Katoliki Michael Maingi Kyengo wazuiliwe hadi Novemba 6, 2019.
Hakimu mwandamizi Bi Hellen Onkwani aliagaza kwamba washukiwa Kavivya Mwangangi na Solomon Mwangangi wazuiliwe katika kituo cha polisi kwa muda wa siku nane ili uchunguzi zaidi kuhusu kifo cha kasisi huyo ukamilike.
Bi Onkwani alipeana uamuzi huu ilhali Bwana Mwangangi alitaka kukiri jinsi mauaji ya kasisi huyo yalivyotekelezwa.
“Badala ya usimulie kisa hicho hapa kortini, nitakuruhusu ufanye hivyo katika kituo cha polisi ukiandamana na watu wa familia yako na wakili ndipo urekodi polepole kilichojiri,” alisema Bi Onkwani.
Mmoja wa maafisa wanaochunguza kesi hiyo, Julio Mutembei alijibu na kumweleza hakimu kuwa mshukiwa alitaka kutoboa siri jinsi Kasisi alivyouawa.
“Naomba hii mahakama irekodi maungamo hayo ya mshukiwa huyu,” alisema Bw Mutembei.
Hata hivyo, hakimu alikatiza huo ushahidi.
Mshukiwa mwingine, Michael Mutunga tayari amezuliwa kwa muda wa siku 10 baada ya kufikishwa mahakamani.
Ijumaa, Mwangangi alisimulia korti jinsi mwendazake alivyofungwa mikono na miguu kabla kuuawa na maiti yake ikafukiwa kando ya mto katika Kaunti ya Machakos.
Alisema kuwa Padri Kyengo alikuwa amefungiwa ndani ya buti la gari.
Alimtaja Mutunga kama rafiki yake wa karibu ambaye alimwomba waandamane akamsaidie ‘kutoa sadaka.’
Alisema pia ni rafikiye ndiye aliyemwamuru kumfunga miguu na mikono marehemu.
“Msiniue tafadhali. Tafadhali usiniue,” Mwangagi alikumbuka jinsi kasisi huyo alimsihi Mutunga aliyekuwa amechukua simu ya Kasisi Kyengo.
Alieleza kuwa alimwamuru amtajie nambari ya siri ya kufungua simu na pesa alizokuwa nazo kwa akaunti.
“Marehemu alimpa Mutunga nambari ya siri ya simu na akaunti za benki,” alisema Mwangagi.
Mshukiwa huyo alisema Mutunga alitoa pesa kwa akaunti ya Kasisi Kyengo kisha akamlaza kifudifudi.
Mahakama iliambiwa Mutunga alichukua panga na kumuua Kasisi.
Bw Mutembei alieleza mahakama kuwa sampuli za marehemu zimepelekwa kuchunguzwa katika maabara ya Serikali.
Pia alisema nguo, gari, simu na kadi za benki zilitwaliwa kutoka kwa washukiwa wanaoendelea kuhojiwa.
Kufikia sasa hakimu alifahamishwa washukiwa watatu wanasaidia polisi katika uchunguzi.