• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Mumias watimuliwa

Wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Mumias watimuliwa

Na SHABAN MAKOKHA

KANDARASI za wafanyakazi wote wa kiwanda cha sukari cha Mumias zimefutwa huku meneja mrasimu akisema anapanga kuajiri wafanyakazi wengine kwa mkataba usio wa kudumu.

Meneja mrasimu, Ponangipalli Venkata Ramana Rao, amesema kwenye ilani ya Novemba 5, 2019, kwamba kampuni hiyo itawatafuta wafanyakazi wapya.

Hatua ya kuwasimamisha kazi imesogezwa nyuma hadi mnamo Septemba 20, 2019, wakati ambapo kampuni hiyo iliwekwa chini ya mrasimu baada ya kulemewa na malimbikizi ya madeni yanayofikia Sh12.5 bilioni ilizodaiwa na Benki ya Kenya Commercial (KCB) na kampuni zingine zinazoidai.

Viwanda vingi eneo la Magharibi vimekuwa vikikumbwa na uhaba mkubwa wa miwa ya kusaga.

Ni hatua ambayo imepingwa vikali na Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Upanzi wa Miwa (KUSPAW), tawi la Mumias wakiongozwa na katibu Vitalis Makokha.

KUSPAW inasema meneja mrasimu alikiuka sheria na kanuni za Leba katika kufuta kandarasi za wafanyakazi hao.

Makokha amesema watu 2,000 ambao walikuwa katika nyadhifa za meneja sasa watasalia kuhangaika.

“Isitoshe, watu hawa wanaidai kampuni Sh1.18 bilioni wakati huu ambapo hawajalipwa kwa zaidi ya miezi 31,” amesema Bw Makokha.

You can share this post!

Bendi ya Qlassic inavyojizolea umaarufu jijini Nairobi

Wabunge waweka masharti mapya dhidi ya mradi wa ujenzi wa...

adminleo