Makala

TAHARIRI: Magavana waelezane ukweli kwenye kongamano

April 9th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

KILA mwaka, magavana hukutana kwenye kongamano la kutathmini hatua walizopiga tangu ugatuzi uanze rasmi mwaka 2013.

Mwaka huu, magavana wanakutana mjini Kakamega, ambapo wanatarajiwa kuangazia kwa kina ufanisi waliopata, na pia yale mambo ambayo yalikuwa changamoto kwa mfumo huo wa utawala, unaopeleka huduma na mamlaka karibu na mwananchi.

Ni katika kutambua hilo, ambapo Wakenya wengi wana imani ya mfumo huo wa uongozi.

Utafiti wa kampuni ya Ipsos unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya Wakenya waliohojiwa walisema wanaridhishwa na utendakazi wa magavana.

Wakenya wengi katika maeneo ya Nyanza na Pwani wanaunga mkono ugatuzi licha ya changamoto.

Baadhi ya changamoto ambazo zinashuhudiwa katika kaunti ni kucheleweshwa kwa pesa kutoka kwa Hazina Kuu.

Hili ni jambo ambalo hufanya kaunti nyingi kulazimika kulimbikiza madeni na wakati mwingine kukosa huduma muhimu kwa kutowalipa wanaosambaza vifaa kwa wakati ufaao.

Kwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa walioalikwa kuhutubu wakati wa kongamano la Kakamega, magavana wanapaswa kumweleza kwa uwazi kuhusu dhiki wanayopata.

Tatizo jingine ni kutumia kiwango kikubwa cha pesa kwa mishahara badala ya maendeleo.

Kaunti zinapaswa kubuni mikakati ya kuziwezesha kuwa na wafanyakazi ambao zinaweza kuwalipa vizuri, lakini wakati huo huo mshahara huo usichukue zaidi ya nusu ya pesa zinazotumwa kwenye kaunti.

Japokuwa Wawakilishi wa wadi wanaonekana kupunguza safari za nje ya nchi, yafaa kuwe na sheria ambapo magavana wataweza kuwadhibiti, bila ya kuangamiza wajibu wa kila upande kuufuatilia mwingine.

Magavana wanapaswa kuwa na uwezo wa kukataa kutishwa na MCA ambao hutaka wafanyiwe mambo yanayokiuka lengo la ugatuzi.

Kwa upande wao, MCA wana jukumu la kuhakikisha kwa hawatiwi mfukoni kiasi cha kutopinga sheria na mapendekezo ambayo yanaweza kumdhulumu mwananchi asipate matunda kamili ya ugatuzi.

Ingawa ni mapema mno kuzungumzia mada zitakazoshughulikiwa kwenye kongamano la mwaka huu, ni muhimu kwa masuala haya kupewa kipaumbele.

Ugatuzi ni wazo ambalo lina umuhimu mkubwa kwa Wakenya na hapana budi ila kuufanikisha.