• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Mpasuko IEBC Chebukati akimsimamisha kazi Chiloba

Mpasuko IEBC Chebukati akimsimamisha kazi Chiloba

Na WAANDISHI WETU

MGAWANYIKO umeibuka upya katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufuatia uamuzi wa Mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati, kumsimamisha kazi kwa muda Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Ezra Chiloba.

Baadhi ya makamishna walipinga uamuzi huo kwenye mkutano waliofanya Ijumaa ambao ulisimamiwa na Bw Chebukati, ambaye baadaye wikendi alisemekana kusafiri kuelekea Nigeria.

Inaaminika anaungwa mkono na makamishna Bw Boya Molu na Prof Abdi Guliye, na kwa upande mwingine anapingwa na naibu wake, Bi Connie Maina na Dkt Paul Kurgat. Bw Chiloba jana alithibitisha kufahamishwa kuhusu hatua iliyochukuliwa dhidi yake kupitia kwa barua pepe ambayo alikuwa ametumiwa Jumamosi usiku.

“Nilipokea barua pepe leo asubuhi ambayo ilikuwa imetumwa Jumamosi usiku, ikisema makamishna walikutana wakaamua niende likizo ya lazima kwa miezi mitatu ili wachunguze ununuzi wa vifaa vilivyotumiwa uchaguzini,” akasema kwenye mahojiano ya simu.

Kulingana naye, hakuelezwa kwa kina kuhusu uchunguzi huo ingawa barua ilitaja “ununuzi wa vifaa muhimu” vya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, na uchaguzi wa marudio wa urais uliofanywa Oktoba 26.

Mwaka uliopita, mgawanyiko ulitokea kati ya makamishna wakati Muungano wa NASA ulipotaka Bw Chiloba asimamishwe kazi kwa madai kwamba alikuwa akishirikiana na Jubilee.

Wakati huo maamuzi ya Bw Chebukati yaliungwa mkono na kamishna aliyejiuzulu, Dkt Roselyne Akombe pekee. Bw Chiloba aliagizwa kwenda likizo kwa wiki tatu akakosa kuhudumia uchaguzi wa marudio wa urais.

 

Ununuzi wa vifaa

Imebainika kwamba kwenye mkutano wa Ijumaa, ripoti mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo ya uchunguzi wa ndani ambao Bw Chebukati aliambia wenzake kuwa ndiye aliyeagiza ufanywe. Ilihusu ununuzi wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

“Ilikuwa ni ripoti ambayo tulikuwa hatujaona ilhali tulihitajika kuichanganua na kuamua kuihusu papo hapo. Mimi na naibu mwenyekiti tulisema haikuwa haki kwani hatukuwa tumeisoma na haikuwa kwenye ajenda ya mkutano,” akasema Dkt Kurgat.

Alisema walipotofauitiana, Bi Maina aliondoka mkutanoni na uamuzi wa mwisho ukafanywa na Bw Chebukati, Bw Molu na Prof Guliye.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Bw Raila Odinga, walipinga zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya OT Morpho kuuzia IEBC vifaa vya ICT kusimamia uchaguzi kidijitali 2017.

Walidai pia Bw Chiloba alishirikiana na maafisa wakuu wa Jubilee na kampuni ya Al Ghurair iliyo Dubai ambayo ilipewa kandarasi ya kuchapisha karatasi za kura, fomu za kujaza matokeo na sajili za uchaguzi.

Kulingana na NASA, kandarasi hizo zilizuia uchaguzi wa haki, na ilikuwa moja ya sababu za Bw Odinga kukataa kushiriki uchaguzi wa marudio.

 

 

 

You can share this post!

Mwanafunzi ajiua mamake kumkera kwa kudai anagawa uroda...

Wanafunzi 5700 waliopata C+ wakosa nafasi katika vyuo vikuu

adminleo