• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 8:55 AM
Klopp amfunza Guardiola gozi la UEFA

Klopp amfunza Guardiola gozi la UEFA

Na CHRIS ADUNGO

LIVERPOOL wamejikatia tiketi ya nusu fainali ya UEFA,Klabu Bingwa Ulaya baada ya kuiengua Man City 5-1 kijumla kufuatia ushindi wao wa 2-1 uwanjani Etihad Jumanne usiku.

Vijana wa Jurgen Klopp wamekuwa mwiba wa Man City katika mikondo yote miwili na walijikakamua na kufuta bao la Gabriel Jesus lililofungwa katika dakika ya pili.

Man City ilimiliki mpira kwa asilimia 69 huku wakiishambulia Liverpool kutoka kila upande lakini ilibidi watosheke na bao hilo moja baada ya refa kuamua Leroy Sane alikuwa ameotea katika bao lake, na Liverpool kuzuia mipira ndani ya kisanduku.

Lakini ilikuwa Liverpool ambao waliamini walikuwa na uwezo wa kulemea vijana wa Pep Guardiola katika kipindi cha pili, hasa baada ya kocha huyo kumkabili refa na kulazimika kutazama mechi akiwa kwa mashabiki.

Mohamed Salah alionyesha makali yake mbele ya goli alipotia kimiani bao la kusawazisha baada ya madifenda wa Man City kushindwa kuondoa mpira uliomponyoka kipa Ederson.

Mbrazili Roberton Firmino alihakikishia Liverpool nafasi katika nusu fainali baada ya kumpkonya mpira Nicolas Otamendi na kupiga bao la hakika lililowafanya mashabiki wa Liverpool kusherehekea kwa njia ya kipekee.

Na ingawa Salah na Firmino walifunga mabao hayo muhimu, mchezaji bora wa mechi hiyo alikuwa James Milner ambaye aliwakaba kwelikweli viungo wa Man City na kuhakikisha nafasi za pasi za mabao zimedidimia.

Ilikuwa mechi ambayo wengi walitarajia Man City ingebadilisha ubao, lakini kocha Jurgen Klopp alimfunza Pep Guardiola jinsi ya kucheza mechi za Klabu Bingwa ulaya. Tumia nafasi zako vizuri kufunga mabao, kumiliki mpira bila mabao ni kazi hewa.

 

You can share this post!

Sofapaka yamtimua Waliaula baada ya Ssimbwa kujiuzulu

Roma yaingia nusu fainali baada ya kuangusha jabali...

adminleo