• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Jinsi washukiwa watatu wa uhalifu walivyouawa Juja

Jinsi washukiwa watatu wa uhalifu walivyouawa Juja

Na LAWRENCE ONGARO

WASHUKIWA watatu wa ujambazi waliovamia kijiji cha Nyacaba, kaunti ndogo ya Juja, wameuawa na maafisa wa polisi.

Inadaiwa ya kwamba kwa muda wa siku chache zilizopita, wakazi wa kijiji hicho wamelalamika vikali jinsi wanavyohangaishwa na wahalifu kila mara.

Afisa mkuu wa polisi Bi Dorothy Migarusha, na naibu wake Abel Mwarania, waliweka mtego katika eneo hilo mnamo Jumanne jioni ili kuwanasa watu hao.

Inadaiwa washukiwa hao walikuwa na gari aina ya pickup nambari KAE 806M ambapo baada ya kutenda uhalifu walijaribu kutoroka.

Hata hivyo, wakazi wa eneo hilo nao walifanya hima na kupiga simu haraka ambapo walielezea hasa mahali washukiwa hao walikuwa.

Bila kupoteza muda, maafisa wa polisi waliojihami walifika mahali hapo na kukabiliana nao ana kwa ana ambapo waliweza kuwaua mara moja.

Washukiwa hao wa ujambazi walijaribu kutoroka baada ya kuona walikaribia kunaswa na polisi lakini juhudi zao zilizimwa baada ya walinda usalama kukabiliana nao bila huruma.

“Tumewapongeza wakazi wa Nyacaba kwa kazi nzuri waliofanya ya kutuarifu kuhusu washukiwa hao watatu ambao wamekuwa wakihangaisha watu. Maafisa wa Polisi nao hawakupoteza muda na kwa haraka walifika hapo,” alisema Bi Migarusha.

Wito wa ushirikiano

Aliwahimiza wakazi hao wawe wakishirikiana na polisi kila mara wanapomshuku mtu yeyote ambaye hawamuelewi vyema.

Baada ya tukio hilo, gari hilo aina ya pickup lilipatikana na mali tofauti iliyoibwa kutoka kwa wakazi hao.

Wakazi hao walionekana kufurahia tukio hilo kwa sababu walisema sasa watapumzika kutokana na vitendo vya majambazi waliozoea kuwasumbua kila mara.

“Tumefurahi kuona ya kwamba polisi leo wameonyesha ujasiri na kupambana na majambazi sugu ambao wamekuwa kero kwetu kwa muda mrefu,” alisema Peter Kamau ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Wakazi wa kijiji hicho walisema siku arobaini za mwizi ziliwadia na kwa hivyo walipongeza polisi kwa kazi nzuri waliyofanya.

You can share this post!

SIRI YA UFANISI: Hakunufaika na mpango wa unyunyiziaji...

AKILIMALI: Waungama, maembe yana pato la uhakika

adminleo