HabariSiasa

ODM: Ruto anavuruga muafaka wa Uhuru na Raila

April 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

VALENTINE OBARA na DAVID MWERE

WABUNGE wa upinzani wamemkashifu Naibu Rais, Bw William Ruto, kwa kupinga pendekezo kuhusu marekebisho ya katiba, wakisema ndiye kikwazo kwa muafaka.

Wabunge sita wa chama cha ODM Jumapili walisema msimamo wa Bw Ruto kupinga uundaji wa nafasi zaidi za uongozi kama vile wadhifa wa waziri mkuu, ni ishara kuwa haungi mkono juhudi za upatanisho zinazoendelezwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Viongozi hao walisisitiza kuwa lazima marekebisho ya katiba yafanywe, Bw Ruto apende asipende.

Wakizungumza katika Kanisa la Church of God lililo katika mtaa wa South B, Kaunti ya Nairobi, wabunge hao walisema matamshi ya Naibu Rais yanaonyesha haungi mkono ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Wakati Wakenya wanapojitahidi kuungana, wengine wanatia bidii kuwatenganisha. Hii haifai. Bw Ruto anafaa ajue tutahamasisha Wakenya ili waunge mkono juhudi zozote za kubadilisha mfumo wa uongozi wakati huo utakapofika,” akasema Mbunge wa Alego Usonga, Bw Samuel Atandi.

Alikuwa ameandamana na Bw Anthony Oluoch (Mathare), Bw George Aladwa (Makadara), Bw Caleb Amisi (Saboti), Bi Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi Mwanamke wa Busia) na Mbunge Maalumu, Bw Geoffrey Osotsi.

Marekebisho ya mfumo wa uongozi yanatarajiwa kuwa miongoni mwa mapendekezo yatakayotolewa kufuatia ushirikiano uliotangazwa mnamo Machi 9, kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Wazo la kuunda nafasi ya waziri mkuu limekuwa likishinikizwa zaidi na viongozi wa kidini ambao wanaamini itakuwa njia ya kuleta uwiano wa kitaifa kwa kuwezesha jamii tofauti kushikilia nyadhifa za uongozi.

 

Salamu si makubaliano

Hata hivyo, Bw Ruto Jumapili alisema ‘salamu’ za viongozi ambao walikuwa mahasimu wa kisiasa hazimaanishi kuna makubaliano ya kuunda nafasi mpya au kugawana mamlaka na watu fulani, huku akitaka viongozi wakome kupigia debe marekebisho ya katiba.

“Wakati wa siasa ulipita na uchaguzi mwingine utafanywa 2022, kwa hivyo inafaa tutumie nguvu zetu kuhudumia wananchi ambao walituchagua,” akasema.

Aliongeza kuwa Wakenya ndio wenye mamlaka ya kuchagua viongozi wanaotaka na jukumu hilo halifai kutolewa kwa watu wachache ikizingatiwa kuwa endapo kutakuwa na nafasi ya waziri mkuu, kuna uwezekano mkubwa atakuwa akichaguliwa na wabunge.

“Wakenya ndio wenye jukumu la kuchagua viongozi wanaotaka kwa msingi wa katiba. Hakuna vile watu wachache bungeni wanaweza kupewa jukumu la kuchagua watu kushikilia mamlaka makuu. Hiyo ni kazi ya wananchi,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Turkana ambako aliandamana na Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen na magavana Josphat Nanok (Turkana), Stanley Kiptis (Baringo), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) na Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Daniel Chemno miongoni mwa wengine.

Hili linatokea siku mbili tu baada ya viongozi wa kanisa Katoliki kupendekeza kuwa katiba irekebishwe ili kuunda nafasi zaidi serikalini kwa nia ya kumaliza uhasama wa kisiasa nchini.