• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
KINAYA: Peleka dhambi zako kwa ‘Baba’ akutakase uwe mweupe pe pe pe!

KINAYA: Peleka dhambi zako kwa ‘Baba’ akutakase uwe mweupe pe pe pe!

Na DOUGLAS MUTUA

USICHEZE na ‘Baba’!

Nilikwambia mwana wa Jaramogi hucheza ligi yake, lakini sijui iwapo uliniamini. Mwache tu, hana mfano wake Kenya. Muulize Sonko.

Ikiwa wewe ni Mkenya kamili anayefuatilia habari za kila siku, huwezi kudai kwamba hujawahi kuona miujiza ikitendeka nchini mwetu. Ipo, fungua macho ujionee.

Kitendawili! Tega. Hujafika Mto Jordan, lakini umemsalimu Joshua ukaoshwa dhambi zako nyekundu kama bendera ukawa mweupe kama pamba.

Najua labda umekosa jawabu, hivyo heri unipe nchi nzima, Kenya, na wala si mji. Jawabu ni salamu za ‘Baba’. Hizo ukipata basi, hulaumiwi tena.

Kila mwanasiasa aliye na matatizo akikutana na ‘Baba’ matatizo yake yanasahaulika kabisa, anakosa hatia kama kitoto kulichozaliwa jana.

Usicheze na mtu aliye na uwezo wa kumsalimu kiongozi wa nchi anayeogopa ujuaji wa naibu wake kutaka kumrithi, jamaa anageuka jasiri na kunguruma kama simba!

Usicheze na mtu anayemsalimu mtu aliyelaumiwa kwa kuiba kura, watu wakapigwa risasi mitaani kutetea wizi huo, halafu ghafla makosa hayo yanafutwa kikamilifu!

Hata wataalamu wa kujumlishia kura kwa njia ya kielektroniki waliodaiwa kutoweka kimiujiza hawakumbukwi tena, wala watoto wachanga waliopigwa risasi za moto.

Usicheze na mtu anayeondoa hofu ya watu walioandamwa kwa kesi ya wizi wa mabilioni ya pesa za huduma ya kitaifa kwa vijana (NYS) mpaka wanajasiria kuwania vyeo vya kitaifa.

Si hayo tu! Japo Bunge, chini ya maelekezo ya ‘Baba’ kabla ya kusalimiana nao, liliwahi kulilia maini ya washukiwa fulani wa NYS, na ‘Baba’ mwenyewe akashtakiwa eti kachafulia watu majina, mashtaka yaliondolewa.

Na tangazo kuu likatolewa eti ‘sisi kina mwana wa mlimani tuko tayari kumpokea ‘Baba’ na kumpa ile sarafu yenye shimo ambayo amekuwa akitafuta miaka hii yote’.

Unakumbuka zile sarafu kuukuu za enzi za ukoloni ambazo zilikuwa na shimo katikati, ambazo kabisa Kenya huru haikuwa na kazi nazo, ghafla wajuaji wakaanza kuzitafuta eti kapata mnunuzi? Hizo sasa…

Umesikia mwenyewe ile meli ambayo imekuwa na nahodha mmoja, ‘Baba’, miaka hii yote juzi haikujua ielekee kusini au kaskazini kuhusu kumfurusha au kumsaza Sonko.

Kisa na maana? Gavana huyo wa Nairobi mwenye matatizo tumbi tele alimtembelea ‘Baba’, akapiga picha mbili tatu, akazitandaza mtandaoni, watu wa ‘Baba’ wakajipata kwenye njia-panda.

Umewahi kujipata katika hali ambapo hujui mkubwa wako anataka nini na unaogopa kumuuliza?

Hapo ndipo unapopeleka mkono mbele kufanya kitu, sauti fulani inakuonya ‘utang’atwa!’ Ukiurejesha tu, nyingine inakwambia ‘mzembe laza damu tu, utakutwa hapo upigwe!’

Usishtuke ukiona Sonko akiponea tu kimiujiza, hata waliotaka kumwangamiza kisiasa wafyate mikia na kuiweka katikati ya miguu wakimwogopa ‘Baba’.

Hilo linawezekana zaidi ikiwa, japo shingo upande tu, Sonko atapanda juu ya jumba la mikutano la KICC na kutangazia kila mtu kwamba ‘Baba’, BBI na ‘Ouru’ ndio Kenya.

Ipo mifano mingi tu ambayo ninaweza kukutolea, wa watu walioingia dhiki kisha wakanusurika kwa kusema ‘Baba’ ndiye mwenyewe-mwenyewe.

Naam, kuanzia watuhumiwa wa ufisadi, mauaji, na mengine mengi. Hata Echesa na rafiki yake, Ole Mashamba wa Sugoi, wakimsalimu ‘Baba’ hutasikia hadithi zao tena.

 

[email protected]

You can share this post!

Ukosefu wa maji washuhudiwa Thika

DINI: Kusitasita ni uzembe unaofanya mambo rahisi kuonekana...

adminleo