Bunge laisuta serikali kwa kutomakinika kuzuia virusi vya Corona
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wameisuta serikali kwa kuruhusu ndege yenye abiria 239 kuingia nchini kutoka China wakisema hiyo inaonyesha kuwa haijajitolea kuzuia kuenea kwa virusi Corona nchini.
Tayari Wizara ya Afya imesema 13 walikuwa ni Wakenya, 198 wakiwa raia wa China huku idadi nyingine ikiwa ya wale wa mataifa mengine waliokuwa wapo safarini.
Wakiongozwa na wabunge ambao ni wataalamu wa kimatibabu, James Nyikal (Seme), Swarup Mishra (Kesses) na Dkt Robert Pukose (Endebess) wabunge hao walisema kuna hatari ya watu hao kueneza virusi hivyo nchini na kuwake Wakenya hatarini.
“Mbona serikali inakataa kuwarejesha Wakenya wenzetu walioko jijini Wuhan, China ilhali inaendelea kuruhusu ndege kutoka taifa hilo kutua nchini? Kuna hakikisho gani kwamba watu baadhi miongoni mwa watu hao 239 hawajaambukizwa ugonjwa huo na huenda pengine wameambukizwa ila tu hawajaanza kuonyesha dalili?” akauliza Dkt Nyikal.
Akaeleza: “Serikali itafahamu vipi ikiwa abiria hao wote watajitenga kwa kipindi cha siku 14, kabla ya kuanza kutangamana na Wakenya? Nimesikia kuwa watu hao tayari wametapakaa kote jijini Nairobi na itakuwa vigumu kwa maafisa wa serikali kuwafuatilia.”
Naye Dkt Mishra ameitaka serikali kuunda Jopokazi la Kitaifa kuhusu Mkurupuko wa Magonjwa (NPPTF) ili iongoze mikakati ya kuzuia kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo humu nchini.
“Jopokazi hilo linafaa kushirikisha maafisa kutoka kwa Wizara ya Afya, Usalama wa Ndani na ile Wizara ya Uchukuzi. Ni jopokazi hilo ambalo litapewa wajibu wa kufanya maamuzi yote kuhusu tatizo hili,” akaeleza.
Kwa upande wake Dkt Pukose alielezea hofu kwamba ikiwa virusi hivyo vitaruhusiwa kupenyeza nchini Kenya itaweza kusababisha maafa makubwa kwa sababu taifa hili halina vifaa na wataalamu waliohitimu kukabiliana nayo.
“Kwa hivyo, tunapasa kuelekeza juhudi zetu kama kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu kwani hatuna uwezo wa kuitibu endapo itagunduliwa nchini. Ikiwa taifa tajiri na lenye uwezo kama China limeshindwa kupata dawa yake, sembuse sisi?” akauliza Dkt Pukose.