Habari Mseto

Mvua itanyesha sehemu nyingi hadi Jumamosi – Utabiri

March 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MERCY MWENDE

KWA siku tano zijazo, maeneo mengi ya nchi yatashuhudia mvua, huku katika baadhi yao, kukiwa na ngurumo za radi.

Idara ya Utabiri wa hali ya hewa, imewashauri wananchi kutumia taarifa yake vyema, na kujiandaa na mabadiliko hayo.

Kwenye taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo, Bi Stella Aura, alitabiri kuwa maeneo ya Kusini mwa nchi, Ziwa Victoria, na mashariki ya Rift Valley yatapata mvua kwa wingi.

Lakini Kaskazini mwa nchi na Pwani kunatarajiwa kuwa na jua na iwapo kutanyesha, yatakuwa manyunyu yatakayoandamana na joto jingi.

“Maeneo karibu na Ziwa Victoria yatatarajiwa kuwa na mvua ya rasharasha nyakati za usiku na mvua itakayoandamana na ngurumo za radi nyakati za alasiri,” ilisema taarifa hiyo.

Katika nyakati za asubuhi, sehemu hizo zitapata jua isipokuwa Jumatano na Alhamisi kutakaponyesha katika sehemu chache.

Katika sehemu ziilizo kwenye Nyanda za magharibi mwa Bonde la Ufa, kutakuwa na mawingu nyakati za usiku isipokuwa Alhamisi ambapo kutashuhudiwa mvua ya manyunyu.

Kaunti hizo ni Turkana, West Pokot na Samburu, katika sehemu hizo kutakuwa na jua isipokuwa Jumatano ambapo kutakuwa na rasharasha nyakati za alasiri na asubuhi.

Kaunti za nyanda za Mashariki za Rift Valley zitashuhudia mvua nyakati za asubuhi isipokuwa Alhamisi na Ijumaa ambapo zitapata jua.

Kaunti hizo ni Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka- Nithi.

Kila siku kaunti hizo zinatarajiwa kupata manyunyu ya mvua nyakati za mchana na usiku.

Eneo la Kaskazini Mashariki ambalo linajumuisha Kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo itashuhudia jua asubuhi na mawingu usiku katika kipindi hicho chote.

Ukanda wa Pwani utapata vipindi vya jua katika nyakati za asubuhi isipokuwa Jumatano na Alhamisi ambapo kutakuwa na mvua ya manyunyu.

Sehemu hizo zitashuhudia mvua ya manyunyu isipokuwa Jumanne na Jumatano kutakapokuwa na vipindi vya jua katika nyakati za mchana.