• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
Nilishauriana na wahusika wote Nairobi, adai Tuju

Nilishauriana na wahusika wote Nairobi, adai Tuju

Na COLLINS OMULO

MABADILIKO ya uongozi katika chama cha Jubilee yaliyotangazwa na Katibu Mkuu, Raphael Tuju kwenye Kaunti ya Nairobi, yaliafikiwa kwa kuhusisha pande zote mbili hasimu.

Imebainika kuwa, Rais Uhuru Kenyatta alihusishwa kwenye kila hatua ya kuafikia orodha hiyo, baada ya mgawanyiko kuibuka kati ya madiwani katika Bunge la Kaunti ya Nairobi.

Uhasama kati ya madiwani ulitokana na ubabe wa kisiasa kati ya Gavana Mike Sonko na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi

Uhasama huo ulikuwa unaelekea kuchacha zaidi baada ya Bi Elachi kuanza kushirikiana na msimamizi mpya wa jiji, Jenerali Mohammed Badi.

Hali hii ndiyo ilichangia wakuu wa Jubilee kuandaa mikutano miwili wiki hii kutekeleza mabadiliko hayo na kuhakikisha chama kiko thabiti bungeni.

Kwenye mabadilko hayo, aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Abdi Guyo ambaye pia ni diwani wa Matopeni, alirejeshewa wadhifa wake.

Upande uliotofautiana vikali na ule wa Bw Guyo nao ulitunukiwa wadhifa wa kiranja wa wengi huku diwani wa Mihang’o, Bw Paul Kados akitwikwa jukumu hilo.

Bw Guyo sasa atachukua wadhifa wa kiongozi kwa wengi kutoka kwa Mwakilishi wa wadi ya Dandora Area 3, Charles Thuo, huku Bw Kados akichukua wadhifa wake kutoka kwa diwani maalumu June Ndegwa

Diwani wa Dandora Area 1, Peter Wanyoike atakuwa Naibu wa Bw Thuo huku Waithera Chege ambaye ni diwani wa South B, akiteuliwa Naibu wa Bw Kados.

Bw Thuo na Bi Ndegwa wamekuwa madiwani wa Jubilee ambao wamekuwa wakiunga mkono Bi Elachi huku Bw Guyo na Bi Chege wakiegemea upande wa Bw Sonko ambaye alitofautiana na Bi Elachi.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Bw Tuju alisema pande zote hasimu zimekubali kufanya kazi pamoja na walijuzwa kabla ya mabadiliko hayo kukumbatiwa.

“Niliteua maafisa wa kushikilia nyadhifa hizo kwa muda hadi waelewane wenyewe. Tulifahamu kwamba kulikuwa na mirengo mbalimbali ndio maana tukasawazisha nyadhifa hizo miongoni mwa madiwani wa pande zote mbili,” akasema Bw Tuju.

Hata hivyo, inaonekana tofauti hizo hazitaisha hivi karibuni, baada ya Bi Elachi kutotambua uongozi mpya wakati wa kikao maalumu cha bunge hilo Ijumaa wiki jana. Alisema bado hajapokea barua rasmi kutoka kwa uongozi wa Jubilee.

“Kama Spika, sijapokea barua yoyote kutoka kwa Jubilee. Nitatambua mabadiliko hayo baada tu ya kupokea barua rasmi ya chama,” akasema Bi Elachi.

Bi Ndegwa naye alidai baadhi ya wakuu wa Jubilee wanaohudumu Ikuluni, ndio walichochea kuondolewa kwao kutokana na ushirikiano waliouanzisha na Bw Badi.

“Hatukuwa tumemaliza mashauriano kati ya pande zote mbili. Bado tulikuwa tunashauriana na hata Bw Tuju alifahamu hilo. Iwapo hii ndiyo njia ya kutuliza uhasama kati yetu, basi ameiongeza zaidi,” akasema.

Mzozo katika kaunti ya Nairobi unaendelea, huku chama hicho cha Jubilee kikikumbwa na msukosuko, unaotokana na hatua ya Bw Tuju kubadili baadhi ya viongozi.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, amewaagiza viongozi wa chama hicho waketi chini na kuafikiana kwanza, kabla ya mageuzi hayo kuidhinishwa.

You can share this post!

Joho ashauri wakazi wajinyime raha msimu wa corona

Niliposikia kifo cha Walibora, mikono yangu iliganda...

adminleo