Habari Mseto

Polisi wafyatuliana risasi na washukiwa wa al-Shabaab Garissa

May 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

POLISI na wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa al-Shabaab walifyatuliana risasi Kaunti ya Garissa baada ya gari la maafisa hao kukwepa kilipuzi kilichokuwa kimewalenga Jumatatu, Kamishna wa kanda ya Kaskazini Mashariki, Nick Ndalana amethibitisha.

Bw Ndalana amesema tukio hilo lilijiri katika eneo la Bura-Mashariki katika barabara kuu ya Garissa-Lapsset.

“Tulipata habari kwamba wapiganaji hao walikuwa maeneo hayo na maafisa wetu wa polisi walikuwa wakishika doria. Baada ya kugundua gari liliepuka kilipuzi – IED – walianza kuwafyatulia risasi maafisa wa polisi,” Bw Ndalana akasema.

Maafisa hao walikuwa wametoka katika kituo cha polisi cha Bura Mashariki.

Bw Ndalana amethibitisha kwamba hakuna majeruhi yoyote yaliripotiwa.

Haya yanajiri siku mbili baada ya al-Shabaab kuharibu kifaa cha mawasiliano cha kampuni ya Safaricom huko Khorof Kharar, Kaunti ya Wajir.

Akithibitisha hilo, mkuu wa polisi wa kaunti hiyo Thomas Ngeywa alisema wapiganaji hao walishambulia kambi ya polisi lakini hawakufaulu.

Jumapili, kikosi cha wanajeshi wa Kenya walifanya mashanbulizi ya hewani wakilenga maficho ya al-Shabaab karibu na mpaka baina ya Kenya na Somalia.