• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Uwanja wa San Siro unaotumiwa na AC Milan na Inter Milan kubomolewa

Uwanja wa San Siro unaotumiwa na AC Milan na Inter Milan kubomolewa

Na CHRIS ADUNGO

NAFASI ya uwanja maarufu wa San Siro ulioko jijini Milan, Italia inatarajiwa kuchukuliwa na uwanja mpya baada ya mamlaka ya turathi za kitaifa nchini humo kutopinga mipango ya kubomolewa kwa uga huo.

Klabu kongwe za AC Milan na Inter Milan zinazoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A) zimekuwa zikitumia uwanja huo kwa pamoja tangu ujengwe mnamo 1926.

Mwaka 2019 vikosi hivyo viwili viliwasilisha kwa pamoja ombi la kubomolewa kwa San Siro na uwanja mpya wenye uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 60,000 walioketi kujengwa karibu na uga huo.

Japo idhini ya maafisa wa mamlaka ya turathi za kitaifa nchini Italia kuhusu kubomolewa kwa San Siro si uamuzi wa mwisho, ni hatua kubwa muhimu katika juhudi za kurasimishwa na kutekelezwa kwa mipango iliyopo.

Kwa mujibu wa maoni ya mamlaka ya turathi za kitaifa kwa Manispaa ya jiji la Milan ambayo inamiliki ardhi ambayo kwa sasa uwanja wa San Siro umejengewa, uga huo hauna vivutio vyovyote vya kitalii wala sifa za kisanii za ujenzi zitakazozuia kubomolewa kwa uwanja wenyewe.

Uwanja wa San Siro umepitia viwango vingi vya ukarabati na ni sehemu ndogo zaidi yenye sifa za ujenzi wa zamani ndiyo iliyosalia katika uga huo.

Wasimamizi wa uwanja wa San Siro, akiwemo Meya wa jiji la Milan, Giuseppe Sala, amepinga vikali hatua ya kubomolewa kwa uwanja wa San Siro na badala yake kupendekeza mpango wa kupanuliwa zaidi kwa uwanja huo ili ufikie viwango vya kisasa badala ya kutumia gharama kubwa kuubomoa na kujenga uga mwingine.

You can share this post!

Kikosi cha Equatorial Guinea kilinifurahisha nikakubali...

Nasa haiwezi kujiunga na Jubilee kwa sasa – Mudavadi

adminleo