Habari Mseto

Mvua inayonyesha kuchangia kushuka kwa ada ya umeme

April 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Gharama ya umeme inatarajiwa kushuka kwa kiasi kikubwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini.

Zaidi, Kampuni ya Kuzalisha Umeme (KenGen) inajishughulisha na zoezi la kuimarisha kiwango cha kawi inayozalisha.

Gharama ya umeme imepanda kwa miezi sita mfululizo kutokana na ukame mkubwa ulioshuhudiwa nchini.

Kutokana na hilo, kiwango cha kawi kilichokuwa kikizalishwa na kampuni hiyo kilikuwa cha chini sana kwa sababu viwango vya maji ndani ya mabwawa ya kuzalisha umeme, hasa bwawa kubwa la Masinga kilikuwa chini sana.

Kutokana na hilo kampuni ya Kenya Power ilikuwa ikisambaza umeme kutoka kwa kampuni za kibinafsi zilizokuwa zikizalisha kawi kwa kutumia dizeli, hali iliyopandishwa bei ya umeme.

Kulingana na Meneja wa KenGen Rebecca Miano, kampuni hiyo inalenga kuongeza kiwango cha kawi inachozalisha na pia kuhifadhi maji kwa lengo la kuwa na kawi ya kutosha hadi mvua fupi.

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika sehemu tofauti nchini inatarajiwa kuendelea mpaka mwishoni mwa mwezi huu kulingana na Shirika la Kutabiri Hali ya Hewa.