Kero la mafuriko Mai-Mahiu
Na ANTHONY OMUYA
Shughuli za usafiri zilitatizika kwa muda wa zaidi ya saa 10 Jumatatu usiku baada ya mvua ya mafuriko kunyesha.
Wasafiri katika barabara ya Mai-mahiu – Nairobi na Narok walilala kwenye magari ya usafiri wa umma, kutokana na mvua nyingi ambayo ilikatiza uchukuzi.
Mvua hiyo hiyo iliyozua taharuki miongoni mwa wasafiri, iliathiri biashara nyingi na kusababisha maporomoko babarani.
Baadhi ya mifugo walisombwa kwa maji ya mvua na kuwaacha wakulima kwa hasara kuu hali ambayo iliacha vinywa wazi wasijue la kufanya.
“Hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda baada ya mvua nyingi. Sio vyema kila siku mvua isababishe maafa ya mifugo na hasara. Suluhisho la kudumu linahitajika. Hii ni fedheha sana. Hasa kwa nchi yetu,” akasema mmoja wa wasafiri Ken Moimbo.
Wasafiri wengi walilalamikia kile walichotaja kuwa kuzembea kwa serikali hasa Wizara ya Uchukuzi.
“Waziri anayehusika anafaa kuanzisha mikakati ya kumaliza tatizo la usafiri katika barabara hii wakati wa mvua, bidhaa nilizokuwa nikisafirisha kwa lori za zaidi ya milioni tano sasa zimeharibika. Ni nani atanifidia ?” akasema Lucy Warimu, mwanabiashara wa mboga ambaye alikuwa akisafirisha bidhaa hizo jjijini Nairobi kutoka kaunti ya Bomet.
Wilson Chacha ambaye alikuwa akisafiri na wanawe watatu wa miaka mitano na kumi, alisema kuwa anahofia kwamba wanawe Huenda wakapatwa na kofu kutokana na baridi kali katika eneo hilo baada ya kulala kwenye basi walilokuwa wakisafiria kutoka Kisii.