• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Baraza laundwa kufungua ibada

Baraza laundwa kufungua ibada

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

HATIMAYE serikali imedhihirisha kujitolea kwake kufungua maeneo ya ibada kwa kubuni baraza maalum la viongozi wa kidini litakaloandaa mwongozo wa kufanikisha mpango huo.

Hata hivyo, ufunguzi huo utatekelezwa kwa awamu huku masharti yaliyowekwa na serikali ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 yakihitajika kuzingatiwa.

Katika tangazo lililochapishwa kwenye toleo maalumu la gazeti la serikali, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na mwenzake wa Afya Mutahi Kagwe, walisema baraza hilo litaongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki dayosisi ya Nyeri, Anthony Muheria.

“Kufuatia agizo lilitolewa na Rais Uhuru Kenyatta katika hotuba yake ya nane kwa Taifa kuhusa janga la Covid-19, na kutokana na mashauriano na viongozi wa madhehebu mbalimbali, tumeteua baraza la viongozi wa kidini watakaoongoza mchakato wa ufunguzi wa maeneo ya ibada,” likasema tangazo lililoidhinishwa na mawaziri hao.

Wanachama wengine wa baraza hilo ni pamoja na Kasisi Rosemary Mbogo, Pasta Samuel Makori, Al Haji Hassan Ole Naado, Sheikh Sukyan Hassan Omar, Sheikh Abdulatif Abdulkarim na Kasisi Joseph Mutie.

Pia kuna Askofu David Oginde, Kasisi Connie Kivuti, Sujata Kotamraju, Kasisi Samuel Thiong’o Mwangi na Sheikh Ali Saidi Samojah.

Hayo yakiendelea, watu 90 zaidi walithibitishwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19, hivyo kufikisha 3,305 idadi ya jumla ya maambukizi nchini.

TF Body text: Hii ni baada ya sampuli 2,419 kufanyiwa uchunguzi ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita. Idadi jumla ya sampuli ambazo zimepimwa nchini kufikia sasa imetimu 108,666

Akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga hilo nchini, Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman alisema wagonjwa 72 zaidi wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Hii imefikisha 1,164 idadi ya wale ambao wamepona corona kufikia Ijumaa.

Kuhusiana na maambukizi mapya Nairobi inaongoza kwa visa 36, Mombasa inafuata kwa visa 34 huku Busia ikishikilia nambari tatu kwa visa 12.

Kutoa damu

Dkt Aman pia alitumia jukwaa la Ijumaa jijini, Nairobi, kuzindua mpango wa kitaifa wa kutoa damu.

Kiwango cha damu inayokusanywa nchini ili kusadia wagonjwa wenye mahitaji kinawakilisha asilimia 1 ya jumla ya idadi ya Wakenya, taifa hili likiwa na takriban watu milioni 50.

Huku Kenya ikijiandaa kuungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha sikukuu ya utoaji msaada wa damu duniani 2020, mnamo Jumapili, inayoadhimishwa Juni 14 kila mwaka, Wizara ya Afya Ijumaa imesema kiwango hicho ni cha chini mno kikilinganishwa na mahitaji ibuka.

Waziri Msaidizi katika Wizara hiyo Dkt Rashid Aman, amesema kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO, kwa mujibu wa idadi jumla ya Wakenya, shirika hilo linapendekeza ukusanyaji wa paili 500,000 za damu kila mwaka, kiwango hiki kikiwa takriban paili 1,370 kwa siku.

Dkt Aman hata hivyo alisema Kenya hukusanya paili 160,000 kwa mwaka, kiwango hiki akikitaja kuwa cha chini mno kikilinganishwa na pendekezo la WHO ili kukithi mahitaji ya damu nchini.

“Kiwango hicho kinaashiria hukusanya paili 450 za damu kila siku. Ni cha chini mno, na kama taifa tunahitaji kufanya busara kukiongeza,” Dkt Aman akasema.

Wakati huu janga la Covid-19 linaendelea kuhangaisha, Wizara ya Afya inasema utafiti unaonyesha kiwango cha utoaji damu ulimwenguni kimeshuka kwa baina ya asilimia 70 na 80.

Hapa nchini, utoaji wa msaada wa damu ambao ni shughuli ya hiari umeshuka kutoka paili 450 hadi 250, Dkt Aman akisema upungufu huo umechangiwa na athari za virusi vya corona.

Hata hivyo, waziri amesema Wizara ya Afya inafanya kila juhudi kuhakikisha upungufu wa damu nchini unaangaziwa.

Akizungumza Ijumaa katika bustani ya ukumbi wa KICC, ambako kampeni ya kuhamasisha watu kujitolea kutoa msaada wa damu imeanza kwa minajili ya maadhimisho ya sikukuu ya usambazaji damu duniani 2020, Dkt Aman alisema serikali imeweka mikakati kabambe kuimarisha shirika la kitaifa kukusanya damu, KNBTS.

“Tumeliongezea wahudumu wengine 22 zaidi. Pia, kwa ushirikiano na Benki Kuu ya Dunia, tutafadhili KNBTS kwa Sh1 bilioni ili kuimarisha huduma zake,” akaeleza, akisema kwamba mikakati iliyowekwa itasaidia kuhakikisha shirika hilo lina vifaa vya kutosha kukusanya damu.

Aidha, aliongeza kusema kwamba serikali na wadau husika, wanapania kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook kuhamasisha wachangiaji kujitokeza kutoa misaada ya damu.

Kufikia sasa, Dkt Aman alisema Kenya ina jumla ya vituo 33 vya kutoa na kukusanya damu.

You can share this post!

Wazee wa Kalenjin wazidi kugawanyika kuhusu Ruto

SIHA NA LISHE: Vyakula muhimu kwa ubongo wa binadamu

adminleo