Habari MsetoSiasa

Ford-Kenya, ANC kuanza mikutano ya Ruto magharibi

June 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON AMADALA

VYAMA vya Amani National Congress (ANC) na Ford-Kenya vimepanga msururu wa mikutano kuanzia leo na wandani wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Magharibi.

Vyama hivyo vinavyoongozwa na Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula mtawalia, vimekumbwa na mizozo ya uongozi katika siku za hivi majuzi, kwani baadhi ya wanachama wanataka viungane na Rais Uhuru Kenyatta lakini wawili hao wamekataa.

Mikutano hiyo, kulingana na wabunge waliozungumza na Taifa Leo, inalenga kupanga mikakati ya kuzima Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

Wawili hao pamoja na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli, hivi majuzi walitangazwa kuwa wawakilishi wa maslahi ya jamii za Magharibi kwa Serikali Kuu.

Mnamo Alhamisi, serikali ya Rais Kenyatta ilionyesha wazi nia ya kushirikiana na kikundi hicho cha Bw Oparanya wakati kamati ya mawaziri inayosimamiwa na Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i ilipokutana nao Nairobi kujadili jinsi ya kukamilisha miradi ya maendeleo Magharibi.

Kando na hayo, Bw Oparanya na Bw Wamalwa wamekuwa wakizuru sana eneo la Magharibi katika siku za hivi karibuni kwa kiasi kinachoonekana kujitafutia umaarufu.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais Ruto, alisema wanataka kuhakikisha kuwa jamii ya Waluhya inapata nafasi katika serikali itakayobuniwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Bw Wetang’ula leo anatarajiwa katika eneobunge la Malava, nyumbani kwa mbunge wa eneo hilo Malulu Injendi, ambapo atakutana na wabunge wa ANC, Ford Kenya na Jubilee. Bw Mudavadi atawakilishwa katika mkutano huo na mbunge wa Lugari Ayub Savula.

“Nimetumwa na chama kumwakilisha kiongozi wetu (Bw Mudavadi). Tunapanga mipango kuhusu jinsi ya kuwafanya Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kuwa maarufu kabla ya uchaguzi wa 2022,” akasema Bw Savula.

Bw Injendi alithibitisha kutakuwa na mkutano lakini hakutoa maelezo zaidi.

Bw Barasa alisema kuwa viongozi hao watapanga mikakati ya kuunganisha jamii ya Waluhya ili wakazi wa eneo la Magharibi waweze kuunga mkono mwaniaji mmoja wa urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

“Mkutano wetu utahusisha viongozi kutoka chama cha ANC, Ford-Kenya na Jubilee. Wabunge wanaoegemea katika kundi jingine (akirejelea Waziri Wamalwa na Gavana Oparanya) hawajakaribishwa mkutanoni,”akasema Bw Barasa.

Bw Wamalwa na Gavana Oparanya ndani ya wiki moja wamezuru katika Kaunti za Bungoma, Busia na Vihiga ambapo wamekutana na wazee na viongozi wa maeneo hayo kujadili miradi ya maendeleo wanayohitaji. Lakini wandani wa Bw Mudavadi na Seneta Wetang’ula wanadai kuwa mikutano ya wawili hao ni ya kisiasa hivyo watahakikisha kuwa wanaizima.

Wanadai kuwa mikutano ya Bw Wamalwa na Gavana Oparanya inalenga kuwahujumu Bw Mudavadi na Wetang’ula, ambao wote wametangaza azma yao ya kuwania urais 2022.

Viongozi hao pia walishutumu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli kwa kutatiza juhudi za viongozi kutoka jamii ya Waluhya kuungana na kuhakikisha kuwa wanakuwa katika serikali ijayo.

“Tunashirikiana na viongozi ambao wanalenga kuhakikisha kuwa jamii ya Waluhya inaungana na kuwa miongoni mwa watakaounda serikali ijayo. Hiyo ndiyo maana viongozi wa ANC, Ford Kenya na Jubilee tumeamua kuungana,” akasema Bw Barasa.