Leba Dei: Makali ya uchumi yawatafuna zaidi Wakenya
Na BENSON MATHEKA
WAKENYA Jumanne waliadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni katika mazingira magumu mno, gharama ya maisha ikiendelea kupanda na idadi ya wasio na ajira ikiongezeka.
Viongozi wa vyama vya wafanyakazi, serikali na waajiri walisikitika kwamba hali ni mbaya nchini hivi kwamba Wakenya wengi wanalazimika kufanya kazi za juakali kupata riziki licha ya kuhitimu katika taaluma mbali mbali.
Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi Bw Francis Atwoli alihusisha hali hiyo na sera hafifu za serikali, ufisadi na mazingira ya kisiasa yaliyoshuhudiwa nchini 2017.
Alieleza matumaini kwamba mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga utaimairisha mazingira ya kisiasa nchini na kufufua uchumi.
“Tunaunga mwafaka wa Rais Kenyatta na Raila Odinga. Kuna haja ya sisi sote kuungana na kujadili hali ya baadaye ya Kenya hii,” alisema.
Alisema kutokana na hali ngumu ya maisha, Wakenya wamekuwa wakihamia mataifa ya nchi za Kiarabu kama Qatar na Saudi Arabia kusaka ajira ambapo huwa wanateswa na kudhulumiwa na waajiri wao na hata kuuawa.
Nyongeza ya 5%
Kwenye hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Leba, Bw Ukur Yattani, Rais Kenyatta aliongeza mishahara ya wafanyakazi wa ngazi za chini kwa asilimia tano.
Nyongeza hiyo ilijiri hata baada ya baadhi ya waajiri kutii agizo la serikali mwaka jana la kuongeza mishahara ya chini kwa asilimia 18.
Bw Atwoli alimtaka Bw Yattani kuhakikisha waajiri ambao hawakutekeleza agizo hiyo wanachukuliwa hatua.
Bw Yattani alisema kwamba atashirikiana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi nchini.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri nchini (FKE), Bi Jackline Mugo alisema hali ni mbaya hivi kwamba maelfu ya Wakenya wanaendelea kupoteza kazi kila mwaka.
Alisema zaidi ya Wakenya 10,000 walipoteza ajira katika sekta ya benki pekee mwaka jana.“Kuna haja ya kuhakikisha Wakenya wanapata kazi zitakazowahakikishia maisha mema siku za baadaye.
Kwa wakati huu wengi wao wanafanya kazi za jua kali ambazo sio za kudumu na haziwezi kuwahakikisha maisha bora,” alisema Bi Mugo.
Kauli ya Raila
Akikiri kwamba Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, Bw Odinga alisema suluhisho sio nyongeza ya mishahara bali ni kuweka mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.
“Mishahara ikiongezwa leo, kesho kodi ya nyumba itaongezeka, nauli itaongezeka na bei za bidhaa muhimu pia zitaongezeka. Suluhu ni kutafuta jinsi ya kupunguzia Wakenya mzigo wa gharama ya maisha ambao umewalemea,” alisema Bw Odinga.
Alisema ufisadi unachangia ukosefu wa nafasi za ajira Kenya. “Kazi zinapotea Kenya kwa sababu ya ufisadi. Tunafaa kuwa na mjadala wa jinsi ya kuimarisha hali hii na ni moja ya masuala ambayo tulikubaliana kushughulikia katika mwafaka wangu na Rais Kenyatta,” alisema.
Bw Odinga alitumia sherehe hizo kusitisha marufuku ya wafuasi wake ya kutotumia bidhaa za kampuni ambazo NASA ilidai zilisaidia Jubilee kuvuruga uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Alisema marufuku hiyo ilichangia kudorora kwa uchumi.