MakalaSiasa

IEBC: Wanaovuna bila jasho

May 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

BENSON MATHEKA na SAM KIPLAGAT

MAKAMISHNA watatu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) waliotangaza kujiuzulu Aprili wanaendelea kupata mishahara yao licha ya kuwa hawafanyi kazi yoyote.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, makamishna hao Consolata Maina, Margaret Mwachanya na Paul Kurgat (pichani) hawapaswi kuendelea kulipwa mishahara yao kwa sababu hawatekelezi majukumu yoyote ya tume.

Kwenye barua aliyomwandikia Katibu wa Wizara ya Fedha, Kamau Thugge na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, Bw Chebukati anasema aliwaandikia barua makamishna hao mnamo Aprili 20 akiwataka waeleze kwa nini hawafiki kazini, lakini hawakujibu barua yake au hata kufika katika ofisi za tume katika jumba la Anniversary Towers, Nairobi.

“Ni wazi kuwa watatu hao wamekwepa kazi kinyume cha sheria,” alisema kwenye hati ya kiapo ya kujibu kesi ambayo mwanaharakati Okiya Omtatah anataka makamishna hao wajiuzulu rasmi.

“Ni maoni ya tume kwamba mshahara wa makamishna hao unafaa kusimamishwa,” inaeleza barua ya Bw Chebukati kwa Dkt Thugge.

Kulingana na Bw Chebukati, kamishna wa tume anaweza kujiuzulu kwa kuandika barua kwa rais, kutoa notisi ya mwezi mmoja au kulipa tume mshahara wa mwezi mmoja iwapo hatatoa notisi. Hata hivyo, anasema watatu hao hawakufuata utaratibu huo.

Anasema ikithibitishwa kuwa walimwandikia rais barua ya kujiuzulu, wanapaswa kuagizwa kulipa madeni na kurudisha mali yote ya tume waliyo nayo.

Kwenye barua hiyo, anawataka makamishna hao warudishe stakabadhi zote na nakala za IEBC, kompyuta, vifaa vyote vya kutoa mafunzo, funguo na pasi za usalama kisha watie sahihi vyeti vya kuonyesha wamerudisha mali hiyo.

Wakikosa kufanya hivyo, anasema, tume italazimika kuwakata pesa kutoka kwa malipo wanayopasa kupata wakiacha kazi.

Makamishna hao walitangaza kujiuzulu wakilalamikia hatua ya Bw Chebukati na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye ya kumsimamisha kazi afisa mkuu mtendaji Ezra Chiloba.

Mshahara wa Bi Maina, ambaye alikuwa naibu mwenyekiti wa tume ni Sh895,270 kwa mwezi na ikizingatiwa kwamba mshahara wa kamishna wa IEBC ni Sh700,000, makamishna hao watatu wamekuwa wakipokea jumla ya mshahara usiopungua 2.5 milioni bila jasho tangu walipotangaza kujiuzulu.

Mbali na mshahara huo unaolipwa na Wizara ya Fedha, wana magari ya serikali, madereva na walinzi ambao kulingana na Chebukati hawajaondolewa kwa vile hawajajiuzulu rasmi.