• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 1:50 PM
Tunatambua Sossion kama kinara wa KNUT – Mahakama

Tunatambua Sossion kama kinara wa KNUT – Mahakama

Na RICHARD MUNGUTI

KITUMBUA cha naibu wa katibu mkuu (SG) wa chama cha kutetea walimu Hesbon Otieno kilitiwa mchanga baada ya mahakama kusema inamtambua tu Bw Wilson Sossion.

Jaji Maureen Onyango alisema katika uamuzi aliotoa Alhamisi kuwa Bw Sossion ndiye kinara wa KNUT na kwamba  mageuzi ama mabadiliko yoyote kwa uongozi wa chama hicho sio rasmi.

Mahakama ilimkubalia Bw Sossion aendelee kuhudumu kama SG hadi kesi aliyowasilishai kupinga kuondolewa kwake kama SG wa KNUT isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Onyango wa Mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi (ELRC) aliharamisha kutambuliwa kwa Bw Hesbon Otieno kama SG mwandamizi wa KNUT.

Bw Sossion aliwasilisha kortini kesi ya kupinga kung’olewa kuwa SG akisema “hatua hiyo itaathiri maslahi ya wanachama zaidi ya 200,000 wa KNUT kote nchini.”

Agizo hilo la Jaji Onyango limesitisha harakati za kumtoa Bw Sossion kuwa SG wa KNUT.

Jaji alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha kuwa msajili wa vyama alimsajili Bw Otieno kuwa SG mpya wa KNUT kabla ya kukabidhiwa agizo la korti likimzuia kufanyia marekebisho sajili.

Msajili alikuwa amemtoa Bw Sossion kuwa SG wa KNUT baada ya kupelekewa majina mapya ya viongozi wa chama hicho kikubwa zaidi nchini cha wafanyakazi.

“ Naamuru Bw Sossion aendelee kuhudumu kama SG wa KNUT. Marekebisho yaliyofanyiwa sajili ya vyama kuhusu mabadiliko ya viongozi wa KNUT hayatambuliwi kwa sasa hadi kesi aliyoshtaki mlalamishi isikizwe na kuamuliwa,” alisema Jaji Onyango.

Bw Sossion aliwasilisha kesi ya kuruhusiwa aendelee kuhudumu kama SG wa KNUT akisema kuna njama za kumtimua kinyume cha sheria.

Bw Sossion anasema kuwa hatua ya kumtimua ni siasa tupu sio eti ameshindwa kutekeleza majukumu yake hata baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge Maalum na chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Kesi  hiyo itasikizwa Mei 28, 2018.

Korti ilielezwa Bw Otieno alisajiliwa kama SG mwandamizi wa KNUT kinyume cha maagizo ya korti Bw Sossion asitimuliwe.

Mawakili Aulo Sowetto na Jackson Awele wanaomtetea Bw Sossion pamoja na Seneta James Orengo waliomba korti isisite kuamuru SG huyo aendelee kuhudumu huku wakiandaa kesi ya kumtaka msajili wa vyama asukumwe ndani miezi sita kwa kukaidi agizo la korti.

“Hata ikiwa Bw Sossion ataendelea kuhudumu kama SG wa KNUT msajili wa vyama hataathirika kwa njia yoyote. Naomba korti iamuru Bw Sossion aendelee kuhudumu,” alisema Bi Sowetto.

Korti ilikuwa imeamuru Bw Sossion aendelee kuhudumu kama SG wa KNUT lakini msajili akamwondoa na kumsajili Bw Otieno ahuhudmu kama mwandamizi.

Bw Otieno alikuwa naibu wa Bw Sossion na aliteuliwa na baraza kuu la chama hicho (NEC) kuhudumu kama SG wa KNUT jambo ambalo Bw Sossion anasema ni kinyume cha sheria.

Mahakama ilikuwa imemwamuru msajili wa vyama asimwondoe Bw Sossion kama SG wa KNUT hadi kesi aliyoshtaki isikizwe na kuamuliwa.

Vile vile Jaji Onyango alikuwa ameamuru KNUT isimwondoe Bw Sossion na kutaka Tume ya kuajiri Walimu (TSC) isitambue SG mwingine ila Bw Sossion.

Uongozi wa Bw Sossion umekumbwa na mtafaruku huku siasa zikienea kuwa anahudumu nyadhifa mbili za umma baada kuteuliwa kuwa Mbunge maalum wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Siasa za kumtimua uongozini wa KNUT zimepamba moto.

Bw Sossion ameshtaki Msajili wa Vyama na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) akiomba korti izuie mtu mwingine yeyote kusajiliwa kuwa SG wa KNUT.

Anaomba korti iamuru asiondolewe kama SG kwa madai anahudumu pia kama Mbunge Maalum.

Akitoa uamuzi Jaji Onyango alisema , “Msajili wa vyama katika afisi ya mwanasheria mkuu amezuiliwa kufanyia marekebisho sajili ya KNUT na kumwondoa Bw Sossion na kuandikisha jina la afisa mwingine kuwa SG,” alisema Jaji Onyango.

Jaji huyo aliamuru Bw Agola ama afisa mwingine yule wa KNUT asiandikishwe kuwa SG.

Jaji huyo alisema kuwa kazi za Bw Sossion hazipasi kutwaliwa na mtu mwingine yule hadi hadi kesi aliyoshtaki isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Onyango pia aliizuia TSC kumtambua SG mwingine wa KNUT ila Bw Sossion.

Azimio la kumwondoa Bw Sossion lilipitishwa mnamo Aprili 30 2018 wakati wa mkutano mkuu wa chama cha KNUT.

You can share this post!

Ajenda Nne Kuu: Kijana airai serikali imkubalie azindue...

Walioshukiwa kumuua kondakta kwa kuongeza nauli waponea

adminleo