Mswada wa Ushuru kupandisha bei ya bidhaa muhimu
Na CHARLES WASONGA
BEI ya unga wa ugali, mikate na mihogo inatarajiwa kupanda ikiwa mswada uliowasilishwa bungeni mwezi Aprili utapitishwa kuwa sheria.
Mswada huo wa marekebisho ya Sheria za Utozaji Ushuru, 2018 unalenga kuwanyima wasagaji uwezo wa kukomboa ushuru wa thamani ya ziada kutoka kwa mahindi, ngano na muhogo.
“Athari ya hatua hii ni kwamba wasagaji hawawezi kukomboa ushuru wa VAT kutoka kwa malighafi na hivyo kupelekea kupanda kwa bei ya unga, gharama ambayo itapitishwa kwa watumiaji bidhaa,” ikasema Chama cha Wasagaji.
Mswada huo unalenga kuanzisha ushuru unaolenga kuongeza ushuru unaotozwa unga wa mahindi, mkate na unga wa muhogo kwa zaidi ya asilimia 10.
Kampuni ya uhasibu PricewaterhouseCoopers (PwC) iliongeza kuwa hatua hiyo ya serikali kutoza ushuru huo utapelekea kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi.
“Ingawa mswada huu utaiondolea serikali mzigo wa kulipa malimbikizi ya ushuru wa VAT, mabadiliko hayo yatachangia ungezeko la bei ya bidhaa nyinginezo,” ikasema PwC.
“Ukweli ni kwamba ikiwa mswada huo utatiwa saini kuwa sheria, maana yake itakuwa kuongezeka kwa bei ya bidhaa za kimsingi kama vile unga, maziwa, mkate….,” ikaongeza kampuni hiyo.
Bei ya mkate imesalia katika Sh50 kwa muda mrefu zaidi na mswada huo, ukipitisha, utapelekea ongezeko la bei yake.
“Serikali inafaa kutafakari upya kuhusu mswada huo wa marekebisho ya sheria za utozaji ushuru. Yatawaathiri Wakenya wengi ambao hutegemea bidhaa hizi za kimsingi ambazo wao hutegemea kila siku,” chama cha wasagaji kilisema kwenye taarifa.