Makala

TAHARIRI: Ufisadi wa kiwango hiki utaiponza nchi

May 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

Matukio ya hivi majuzi nchini yamedhihirisha uozo ambao umekithiri katika taifa ambalo limekumbwa na visa mbalimbali vya utovu wa maadili.

Ripoti kuhusu wizi wa Sh9 bilioni za NYS, wizi wa moyo wa mfu na vifo vya raia wasio na hatia katika mkasa wa Solai ni baadhi ya visa vinavyotamausha na labda kuonyesha jinsi maovu yameshamiri kotekote.

Tangia nyakati za sakata ya Goldenberg, wizi wa pesa za kiwango cha mabilioni umekuwa gumzo la kawaida, lakini twajua hasa bilioni ni nini?

Iwapo mtu hulipwa Sh3m kwa mwezi, itamchukua muda wa miaka 30 kupata Sh1 bilioni. Itamchukua anayepata Sh1 milioni kwa mwezi miaka 80 kuunda Sh1 bilioni.
Hivyo basi, inastaajabisha na kuhuzunisha kwa jinsi mtu anaweza kuiba Sh9 bilioni kwa wakati mmoja bila haya wala hofu yoyote.

Hawa ni watu wasiojali hali halisi ya maisha wanayopitia Wakenya wa kawaida. Inaonesha hali ya kutojali ya watu hawa wasio na chembe cha utu.

Kuhusu kuibwa kwa moyo wa mfu, ni ukosefu wa maadili na utu hata kuzungumzia suala hili.

Tunasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu jambo hili lakini linalokeketa maini zaidi ni kwamba, ni kwa namna gani mtu anaweza kuwazia kung’oa baadhi ya sehemu za mwili wa mfu pasi na idhini ya jamaa au wosia wake?

Yawezekana kwamba mtu kama huyo husukumwa na uroho na tamaa ya pesa na kupata utajiri wa haraka. Hapo awali kulishamiri ripoti za kutoweka na kuuawa kwa zeruzeru ambao hupatikana bila ya baadhi ya sehemu za miili yao.

Yadaiwa kwamba sehemu hizo huuzwa kwa wachawi ili kuendeleza shughuli zao za uganga. Hili linasikitisha mno.

Kuhusu mkasa wa Solai, maisha yamepotea na jamaa wamesalia na mahangaiko tele. Ni msiba ambao umeathiri kila Mkenya.

Ziara ya rais na naibu wake eneo hilo ilidhihirisha umoja wa Wakenya hasa kunapotokea msiba wa aina hii.

Pana haja ya kusanifu mabwawa yanayojengwa ili kuepushia jamii janga kama la Solai.

Wakenya hawana budi kuzuia majanga haya kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni Wakenya wanaoishi maisha ya kawaida na vizazi vijavyo.