• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Ripoti: Wanaume walipigwa zaidi na wanawake kipindi cha corona

Ripoti: Wanaume walipigwa zaidi na wanawake kipindi cha corona

Na WANDERI KAMAU

WANAUME wengi walipigwa ama kutukanwa na wapenzi wao walipokuwa wakikaa nyumbani kutokana na kanuni za kukabili virusi vya corona kati ya Machi na Septemba.

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Trends and Insights for Africa (TIFA), unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanaume walitandikwa, kutukanwa ama kupitia yote mawili kipindi hicho maarufu kama ‘lockdown’.

Ripoti hiyo inasema idadi ya wanaume waliodhulumiwa ilikuwa ya juu ikilinganishwa na ya wanawake waliopigwa ama kutukanwa.

“Hili linaonyesha kuwa kinyume na dhana nyingi, wanaume wengi walipitia dhuluma mikononi mwa wapenzi wao. Hili lilisababishwa pakubwa na changamoto za kiuchumi, ikizingatiwa kuwa wengi ndio wanaotegemewa na familia zao,” akasema Bi Ireri

Akitoa matokeo hayo jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa TIFA, Maggie Ireri, alisema kando na wanawake na wanaume kudhulumiwa, watoto pia walijipata katika hali hiyo.

Tangu janga la corona liliporipotiwa nchini mnamo Machi, kumekuwa na ongezeko kubwa la dhuluma za kinyumbani kati ya jinsia zote mbili katika sehemu mbalimbali nchini.?Utafiti huo unaeleza kuwa licha ya wanafunzi kurejelea masomo yao Jumatatu, wazazi wengi wana hofu kuwa huenda wanao wakaambukizwa virusi vya corona wakiwa shuleni.

Utafiti ulionyesha kuwa karibu robo tatu yao wana hofu hiyo, huku wanawake wakiwa wengi ikilinganishwa na wanaume.

Tangu Jumatatu, baadhi ya wanafunzi waliripotiwa kurudi shuleni mwao bila barakoa, hali inayoongeza wasiwasi kuhusu usalama wao.

Baadhi ya wazazi walieleza tashwishi kuwaruhusu wanao kurejea shuleni, wakisema bado hawajapewa hakikisho kuhusu usalama wao.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu George Magoha alipuuza baadhi ya hofu hizo, akisisitiza serikali imefanya kila juhudi kuhakikisha wanafunzi hawaambikizwi virusi.

Vile vile, imebainika kwamba ni robo mbili pekee ya wakazi katika mitaa duni ambao watoto wao walikuwa wakipata masomo kwa njia ya mtandao wakati shule zilipokuwa zimefungwa.

Hili ni licha ya serikali kusisitiza kuwa ni idadi ndogo tu ya wanafunzi nchini ambao walikuwa hawapati masomo hayo.

Utafiti ulionyesha kuwa zaidi ya thuluthi moja ya watoto walitegemea televisheni na simu huku idadi ndogo sana ikitegemea redio.

You can share this post!

RIZIKI: Biashara ya mboga kienyeji yamfaa pakubwa

Msinidharau Mswambweni – Kalonzo