Habari

Mwanamke ndani miaka 15 kwa kunajisi tineja

May 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RUSHDIE OUDIA

KATIKA kisa kisicho cha kawaida, Mahakama ya Kisumu Jumatano ilimhukumu mwanamke wa miaka 24 kifungo kikali cha miaka 15 gerezani kwa kufanya mapenzi na mvulana tineja wa miaka 15.

Hukumu hiyo ilizua mjadala mkali miongoni mwa watumizi wa mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kwani mara nyingi visa vingi kuhusu ubakaji na unajisi huhusisha wanaume kuwadhulumu wasichana na wanawake.

Bi Judith Wandera (pichani) alipatikana na hatia ya unajisi na kumfanyia mtoto kitendo kichafu kinyume na sheria mnamo Julai 5, 2017 katika Kaunti ya Kisumu.

Mashahidi saba walitoa ushahidi dhidi yake kwenye kesi hiyo huku Bi Wandera akijitetea kivyake.

Kwenye uamuzi wake, Hakimu Mkuu wa Kisumu, Bi Joan Wambilyanga alisema wawili hao walikamatwa Julai 17, mwaka mmoja baada ya kuanza uhusiano wa kimapenzi.

“Wote wawili walikiri kushiriki mapenzi, wakati mwingine walitumia kinga na wakati mwingine hawakutumia,” akasema Bi Wambilyanga alipokuwa akitoa hukumu.

Akijitetea, mshtakiwa alidai hangeweza kujua umri wa mvulana huyo walipokutana kwani alipomtazama hakuonekana kama mwenye umri wa chini ya miaka 18, na pia alikuwa ni mwendeshaji wa bodaboda.

Sheria inayohusu makosa ya vitendo vya ngono huruhusu mshtakiwa kujitetea kuwa hakufahamu umri wa mtu kutokana na maumbile, lakini mahakama ilipata kuwa Bi Wandera hakuweka juhudi zozote kubainisha umri wa tineja huyo.

Hakimu alipuuzilia mbali tetesi za mshtakiwa na kumwambia angethibitisha iwapo alichukua hatua yoyote kutambua umri wa mlalamishi.

“Hapakuwa na ushahidi wowote kuonyesha kuwa mlalamishi alidanganya kuhusu umri wake na utetezi wa mshtakiwa umetupwa nje kwa sababu alishindwa kuthibitisha hatua alizochukua kubainisha kama mvulana huyo alikuwa na umri wa chini ya miaka 18,” akasema Bi Wambilyanga.

Mshtakiwa aliambia korti kuwa tineja huyo alikuwa akitumia dawa za kulevya na alionekana tu mwenye umri mdogo alipokuja mahakamani kutoa ushahidi.

 

Aliacha masomo

Katika ushahidi wake, tineja huyo alieleza mahakama jinsi alivyoacha shule alipokuwa katika darasa la saba mwaka wa 2016 na akawa mhudumu wa bodaboda.

Hakimu alisema wawili hao walikamatwa mara mbili awali, mshtakiwa akaambiwa akomeshe uhusiano huo baada ya mama ya mvulana kulalamika kuhusu tofauti ya umri wao lakini mshtakiwa akapuuza hayo yote.

Bi Wandera aliomba asamehewe kwa sababu ana mtoto, kaka na mama ambao wanamtegemea kimaisha. “Mimi pekee ndiye ninategemewa. Tafadhali nisamehe sitarudia kosa hilo,” akaomba. Lakini ombi lake halikufua dafu.

Hukumu iliposomwa alijikuna kichwa huku macho yake yakionekana kana kwamba alitaka kulia, kisha akamtazama dadake aliyekuwa mahakamani.
Wakati wote kesi ilipokuwa ikisikilizwa, Bi Wandera alikuwa mtulivu lakini hukumu iliposomwa alibadilika kwani ni kama hakutarajia adhabu kali kiasi hicho.