NYS yafaa kuvunjwa na fedha hizo kufadhili elimu – Moses Kuria

NA PETER MBURU

WAKENYA kupitia mitandao ya kijamii wamechangamkia pendekezo la mbunge mtatanishi wa Gatundu Kusini Moses Kuria kuwa serikali ielekeze Sh16 bilioni ambazo inatumia kufadhili tume ya huduma kwa vijana (NYS) katika miradi mingine.

Kulingana na Bw Kuria pesa hizo zitakuwa na manufaa endapo zitaelekezwa kuinua miradi kama ya kujenga taasisi za mafunzo ya kiufundi, ili kila eneobunge liwe na angalau moja.

Mbunge huyo anapendekeza kuwa baada ya kufanya hivyo, serikali inaweza kugeuza taasisi hizo kuwa za NYS ili kila eneobunge liwe na tawi lake.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, mbunge huyo amependekeza kuwa serikali itumie mabilioni hayo ya pesa ambazo mwishowe huishia kuporwa kufadhili ujenzi wa taasisi katika maeneobunge zaidi ya 150 ambayo aidha hayana ama ujenzi wake unaendelea.

“Tuna maeneobunge 60 yaliyo na taasisi za TTI, 70 ambapo ujenzi unaendelea na 85 ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2018-2019 na hivyo kuwacha maeneobunge 75 pekee bila taasisi za TTI kufikia Juni 2019,” akachapisha Bw Kuria.

“Wazo langu ni kuwa Sh16 bilioni zielekezwe kutoka kwa NYS ili kumaliza ujenzi wa taasisi za TTI kwenye maeneobunge yote 290, kisha kufanya kila ya taasisi hizo taasisi ya NYS katika kila eneobunge. Kisha NYS ivunjwe,” mbunge huyo akaendelea.

“Ikiwa lazima tuwe na ufisadi ndani ya NYS, wacha tuwe na vitengo 290 vya ufisadi nchini,” Bw Kuria akasema.

Semi za mbunge huyo zilikumbana na maoni mengi tofauti kutoka kwa wakenya, wengi wakimuunga mkono, wengine kukosoa na wengine kumtaka aziwasilishe kama mswada bungeni.

Maoni ya Wakenya aidha yaliakisi namna walivyokerwa na ufisadi unaoendelea katika taasisi tofauti za serikali, wakikemea uozo wa maadili miongoni mwa maafisa wengi.

“Mbona usiwasilishe bungeni ambapo wabunge wataunga mkono ikiwa unamaanisha maneno yako Kuria, wakenya wamechoshwa na kurushiana lawama,” akasema Hon Shiloh.

“NYS sio tatizo, wezi ndio shida, kila unapopeleka pesa wataiba. Tunahitaji sio tu mabadiliko katika uongozi, bali pia mabadiliko kamilifu ya imani na itikadi za kisiasa,” akasema Gichuru Gaitho.

Habari zinazohusiana na hii