SAKATA YA NCPB: Kiunjuri akiri wakulima bandia walivuna wasipopanda
Na LUCY KILALO
WAZIRI wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri Jumatano alikiri kuna wahusika wakuu wa kashfa ya mahindi kando na wale walioorodheshwa kulipwa kwa mahindi waliyopeleka kwa depo za Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).
Hata hivyo, alikosa kuwataja majina akisema ukweli hatimaye utajitokeza katika ukaguzi wao. Waziri aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo kuwa, lazima kuna wahusika wakuu waliowasaidia waliosambaza mahindi ambao walilipwa mamilioni katika muda usiozidi wiki moja
“Kuna watu wakubwa wanaohusika kuwasaidia kulipwa kwa muda wa siku tatu hadi tano. Ukweli utajitokeza tu lakini naweza kuwahakikishia kuwa si afisi yangu,” alisema.
Bw Kiunjuri alitoa mfano wa mkulima ambaye alifanya safari zaidi ya 700 kwa bohari la Eldoret katika muda wa miezi mitatu, na kupeleka magunia zaidi ya 200,000 ya mahindi na kulipwa zaidi ya Sh330 milioni.
Pia alirudia kusema hakuna pesa zimepotea na hilo litabainika tu wakihesabu magunia ya mahindi moja moja katika depo zake zilizopokea mahindi. Kamati hiyo inatarajia ripoti yake katika muda wa siku 21 zijazo.
Mbunge wa Moiben, Silas Tiren alipendekeza uchunguzi ufanywe kuhusiana na maisha ya wakulima hao ili kuweza kubainisha ikiwa ndio walionufaika na pesa hizo, ama kufanya hivyo kwa niaba ya watu wengine.