Ruto akerwa na bei ghali ya mashamba jijini Nairobi
Na VALENTINE OBARA
Naibu Rais William Ruto amelalamikia bei ghali ya mashamba jijini Nairobi.
Akizungumza Jumanne katika ukumbi wa KICC, Nairobi wakati wa uzinduzi wa sera mpya ya usimamizi wa mashamba ya taifa, Bw Ruto alisema usimamizi mbaya wa ardhi ndio hufanya bei kuwa ya juu kupita kiasi mbali na kuibua changamoto zingine kama vile ueneaji wa mitaa ya mabanda na unyakuzi wa maeneo muhimu ya kutunza mazingira.
“Katika baadhi ya maeneo Nairobi ambako bei ya ardhi ni kati ya Sh500 milioni na Sh600 milioni kwa ekari moja, ni kutokana na mipangilio mibaya na ukosefu wa mwongozo wa wazi kuhusu matumizi ya ardhi,” akasema.
Kulingana na Bw Ruto, sera hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi na Mipango ya Ujenzi itasaidia pia kukabiliana na uchipuzi wa mitaa ya mabanda na kudhibiti bei ya ardhi ambayo kulingana naye imekuwa ya juu kupita kiasi.
Kati ya Sh17 bilioni zinazonuiwa kutumiwa kwa utekelezaji wa sera hiyo, imependekezwa Sh4 bilioni zitumiwe kurudisha hali halisi ya ardhi zilizo katika maeneo ya kuvutia mvua na za ufuoni.
“Tunatarajia kuona serikali kuu na za kaunti zikiunda mipango ya utumizi wa ardhi. Sera hii lazima isaidie kuunda mbinu za usimamizi bora wa ardhi kwa njia ya uwazi, uwajibikaji na inayoshirikisha wadau wote,” akasema.
Waziri wa Ardhi Bi Farida Karoney, alisema itasaidia serikali kufanikisha malengo yake makuu ya maendeleo hasa katika uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi na ujenzi wa nyumba bora za bei nafuu mijini.