Wandani wa Ruto walia vita dhidi ya ufisadi vinalenga kusambaratisha ndoto yake 2022
Na LEONARD ONYANGO
WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wameendelea kudai kuwa vita vilivyopamba moto dhidi ya ufisadi ni njama inayomlenga ili kumharibia sifa asiwe rais 2022.
Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen kuwa vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi ni njama ya kuzima ndoto ya Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022.
Pia alisema tangazo la Rais Uhuru Kenyatta kuwa watumishi wa umma watatakiwa kufafanua walivyopata mali yao, pamoja na ushirikiano kati ya rais na kiongozi wa ODM Raila Odinga ni kati ya mbinu zinazolenga kumzima Bw Ruto.
Msimamo wa Bw Murkomen unalingana na wandani wengine wa Bw Ruto, Seneta wa Nandi Samson Cherargei na wabunge Nelson Koech (Belgut) na Oscar Sudi (Kapseret), ambao wameshikilia kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga watu wachache kwa sababu za kisiasa na wala si kwa manufaa ya Wakenya.
Bw Murkomen, na ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Ruto, alisema vita dhidi ya ufisadi vinatekelezwa kwa lengo la kumpaka tope Naibu Rais ili kudidimiza umaarufu wake.
Kulingana na Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet, juhudi hizo, ambazo zimeshika kasi katika siku za majuzi, ni njama ya washauri katika Ofisi ya Rais kusambaratisha ndoto ya Bw Ruto kuingia Ikulu.
“Walipogundua kwamba umaarufu wa Naibu Rais unaongezeka kwa kasi nchini waliketi chini na kutafuta mbinu za kumzima. Vita dhidi ya ufisadi ni miongoni mwa mbinu walizobuni ili kumchafulia sifa,” Bw Murkomen aliambia runinga ya Citizen mnamo Jumapili.
Alisema watu hao, ambao hakuwataja, wametumia raslimali nyingi kuhakikisha kuwa Bw Ruto hatakuwa rais 2022.
“Lengo lao ni kuzua uhasama na mgawanyiko baina ya Rais Kenyatta na Bw Ruto,” akasema Bw Murkomen.
Alidai kuwa wito uliotolewa na Rais Kenyatta wa kutaka watumishi wa serikali kufafanua walivyopata mali yao ni miongoni mwa njama za kumzima Bw Ruto.
“Tumefanya uchunguzi na kubaini kuwa stakabadhi iliyokuwa na pendekezo la kutaka utajiri wa watumishi wa umma uchunguzwe iliandaliwa na watu hao wanaompinga Bw Ruto,” akasema Seneta huyo.
Alisema mrengo wa Bw Ruto haukushauriwa kuhusiana na mpango huo wa kutaka kuchunguza utajiri wa watumishi wa umma. “Wito wa kutaka kuchunguza utajiri wa watumishi wa umma unalenga mtu mmoja ambaye ni Naibu wa Rais,” akadai.
Alieleza pia kuwa hatua ya Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta ni njama ya kusambaratisha chama cha Jubilee.
“Lengo la Rais Kenyatta lilikuwa kuunganisha nchi lakini lengo kuu la Bw Odinga lilikuwa kubomoa Jubilee,” akadai.
Seneta huyo pia alieleza kuwa mrengo wa Bw Ruto ulishtushwa na kauli ya Rais Kenyatta aliyotoa akimrejelea naibu wake kama “Kijana wa Kutangatanga’.
“Rais alipotoa kauli hiyo tulishtuka. Hatufai kufuata mkondo huo wa kudunisha baadhi ya viongozi,” akasema.
Bw Murkomen, hata hivyo, alisisitiza kuwa uhusiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Ruto ungali imara.