Makala

ULIMBWENDE: Njia rahisi za kutokomeza chunusi usoni

July 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

CHUNUSI ni ugonjwa wa ngozi unaowaathiri watu wengi katika kipindi fulani cha maisha yao; hasa wanapobaleghe.

Ugonjwa huu husababisha vipele vidogo vya mafuta kwenye ngozi na wakati mwingine hufanya ngozi kuwa na maumivu au kuhisi kuungua.

Vipele hivi hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinazibwa kwa mafuta na seli za ngozi zilizokufa au bakteria.

Mara nyingi chunusi hutokea usoni, mgongoni, kifuani na shingoni na huwaathiri watu wenye umri kati ya miaka 11-30.

Huathiri zaidi wasichana kuanzia umri wa miaka 14-17 na wavulana kuanzia umri wa miaka 16-19.

Kawaida ngozi ina vishimo vidogo vidogo vya kutolea jasho, mafuta na seli zilizozeeka kutoka ndani ya mwili.

Katika ngozi pia kuna tezi ya mafuta iitwayo ‘sebacous gland’ inayotoa mafuta yaitwayo sebum.

Uzalishaji wa sebum nyingi na seli za ngozi zilizokufa husababisha kuziba kwa vishimo vidogo vidogo vya ngozi vinavyopitisha jasho katika ngozi na kusababisha chunusi.

Kando na hayo, chunusi pia huchangiwa na sababu nyinginezo kama:

  • Mabadiliko ya homoni
  • Bakteria
  • Matibabu
  • Vinasaba (genetics)

Kuna njia nyingi za matibabu za kupunguza chunusi kama kubadili hali ya maisha, na kujipaka dawa.

Usijaribu kuviminya au kuvisugua kwa nguvu vipele kwa sababu hufanya ngozi kuuma na kutengeneza makovu ya kudumu.

Jiepushe kutumia manukato au vipodozi kwenye ngozi yenye chunusi.

Tumia bidhaa za urembo zisizoziba matundu madogo madogo ya ngozi yako.

Chunusi pia huweza kutibiwa kwa matumizi ya tiba asili kama matumizi ya matunda na viungo kama vitunguu saumu, mdalasini na vingine.

Hii ni njia nzuri ya kupatia ngozi unafuu na tiba mbadala na inayofaa katika ngozi yako. Zifuatazo ni baadhi ya tiba za kiasili za chunusi na salama kwa ngozi yako:

  1. Mdalasini uliosagwa na asali

Tumia mchanganyiko wa asali na mdalasini wa unga kwa kupaka angalau mara moja kwa siku. Asali na mdalasini zinasaidia katika uponyaji kwa sababu zina ‘anti-bacteria’ (zinaua na kuzuia bacteria) Jinsi ya kufanya:

  • Chukua asali kwenye kipimo cha vijiko vitatu vya chai
  • Chukua mdalasini wa unga kwa kipimo nusu kijiko cha chai
  • Changanya pamoja
  • Paka sehemu yenye chunusi na kisha kaa na mchanganyiko huo kwa angalau dakika 10-30 kisha osha kwa maji ya uvuguvugu

Mdalasini unaweza kuwasha kwenye ngozi hivyo unashauriwa ujaribu kupaka kidogo kwenye kiganja cha mkono kwanza ili kupata uhakika kua haitakusumbua.

2. Matango

Unaweza kutumia tango kwa kuondoa chunusi na hata kuondoa mabaka katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuonekana yenye afya na yenye kuvutia.

Matango ni mazuri sana kwa kusafishia uso na hasa ukiwa na chunusi. Kata tango na ulimenye kisha paka usoni. Acha likae kwa muda wa dakika 15 hadi 20 hivi, kisha suuza kwa maji baridi.

Unaweza kurudia kwa siku mara mbili mpaka mara tatu hadi utakapopona.

3. Asali

Matumizi ya asali kutibu chunusi huwezesha ngozi, iwe na afya na nyororokwa sababu kwenye asali, kuna virutubisho vingi vyenye kazi ya kuua bakteria na kuzuia uchafu kwa ngozi.

Weka asali kidogo katika sehemu ilioathirika na uache kwa muda mrefu uwezavyo. Unaweza kupaka kwenye uso mzima au hata mwili mzima ukitaka kwa sababu asali inarutubisha ngozi ya mwili na kuifanya iwe na afya na mwonekano mzuri.

Ukisha ridhika na muda wa asali kwenye ngozi yako unaweza kusafisha kwa kutumia maji ya fufutende.

4. Papai

Matumizi ya papai yameonyesha matokeo mazuri sana katika kuondoa chunusi usoni na kusafisha sehemu zingine za mwili.

Pondaponda kiasi kidogo cha papai na upake palipo na chunusi. Acha papai pahala ulipopaka kwa muda mrefu iwezekanavyo.

Ukisha ridhika na muda huo unaweza kujisafisha kwa kutumia maji ya kawaida. Unaweza kurudia mara kadhaa kila siku kama ukitaka.