HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Mama akamatwa kwa kuzuia mwanawe kufanya mtihani, adai nambari ‘666’ni ya kishetani

Na WAANDISHI WETU October 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAMA mmoja mwenye umri wa miaka 38 amekamatwa kaunti ya Mombasa baada ya kumfungia binti yake nyumbani na kumzuia kufanya mtihani wa kitaifa wa KPSEA kwa madai kuwa nambari yake ya mtihani ilikuwa na tarakimu za kishetani, 666.

Mama huyo wa watoto watano alikamatwa Jumanne baada ya mwanawe kukosa kufika katika kituo cha mtihani cha shule ya msingi ya  Kwa Jomvu. Alidai kuwa uamuzi wake ulitokana na maagizo aliyopokea kutoka kwa Mungu.

“Mimi ni mtu ninayemcha Mungu, mtumishi wake na mhubiri. Nilizungumza na Mungu, akanionyesha kuwa nambari ya mtihani wa binti yangu haikuwa sahihi,” alisema akiwa katika Kituo cha Polisi cha Jomvu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bakari Mwerephe, alisema mwanafunzi huyo alikuwa amefanya mtihani wa siku ya kwanza Jumatatu, lakini mama yake akampigia simu akisema hataruhusiwa kuendelea na mitihani kwa sababu ya nambari hiyo.

Shangazi wa msichana huyo aliarifu polisi na maafisa wa Idara ya Watoto, ambao walifika nyumbani saa tatu na nusu asubuhi na kumuokoa mwanafunzi huyo akiwa amevalia sare za shule. Alisindikizwa hadi kituoni na kuruhusiwa kufanya mtihani.

Kamanda wa Polisi wa Jomvu, Selina Chirchir, alisema maafisa waliingilia kati ili kuhakikisha haki ya mtoto ya kupata elimu inalindwa.

Binamu wa mama huyo, Juliet Ndewa, alisema familia imekuwa ikipambana na kile ilichokitaja kuwa msimamo mkali wa kidini unaoathiri watoto. Mwezi mmoja uliopita, mama huyo alikuwa ameitwa na maafisa wa watoto baada ya kuripotiwa kuwazuia watoto wake kwenda shule na kutafuta matibabu wanapougua.

Mama huyo anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa afya ya akili na kuhojiwa zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazohusiana na kupuuza malezi na  haki ya mtoto kupata elimu.

Katika habari nyingine, wanafunzi watatu wa kike wanafanya mitihani ya KJSEA hospitalini kaunti ya Bomet. Wawili walijifungua siku ya kwanza ya mitihani, huku mwingine akifanya mtihani katika Hospitali ya Tenwek baada ya kujifungua.

Huko Nakuru, watahiniwa 27 ambao majina yao hayakuwa kwenye orodha rasmi waliruhusiwa kufanya mitihani maafisa wa Baraza la Mitihani la Kitaifa (KNEC) walipoingilia kati. Walijumuisha watahiniwa 11 wa KPSEA na 16 wa KJSEA.

Hata hivyo, mwanafunzi mmoja wa KJSEA katika Shule ya Kionduso PAG, Kisii, alikosa mtihani baada ya kubainika kuwa hakuwa amesajiliwa. Babake, Dickson Asiago, alitaka Wizara ya Elimu ichukue hatua dhidi ya waliohusika.

Wakati huohuo, usalama umeimarishwa katika maeneo yanayokumbwa na ujangili katika kaunti za Samburu, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Turkana na Baringo ili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mitihani bila hofu.

KPSEA inatarajiwa kukamilika kesho, huku mitihani ya KJSEA ikiendelea hadi Ijumaa.