Vita kati ya magavana na Ruto kuhusu maendeleo vyatishia ugatuzi
MVUTANO kati ya Rais William Ruto na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuhusu nani anastahili sifa za miradi ya maendeleo umeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa ugatuzi, huku viongozi wakishindana kudhibiti na kumiliki kisiasa miradi inayolenga kuwahudumia wananchi.
Wiki iliyopita, Bw Natembeya alimlaumu Rais kwa kujipa sifa za miradi inayofadhiliwa na serikali ya kaunti, ikiwemo Soko la Masinde Muliro mjini Kitale.
Gavana huyo alisema serikali ya kaunti, kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, ilitumia zaidi ya Sh800 milioni kujenga soko hilo, huku serikali ya kitaifa ikichangia Sh56 milioni kukamilisha kazi zilizobaki.
Pia alipinga ujenzi wa hospitali ya thamani ya Sh1 bilioni, akisema hakushirikishwa kabla ya mradi huo kuanzishwa. Rais, aliyezindua ujenzi wa hospitali hiyo yenye vitanda 300, alimshutumu gavana kwa kuzuia maendeleo ya huduma muhimu za afya.
Hata hivyo, wataalamu wanasema mzozo huo ni sehemu ya vita pana kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhusu ufadhili, utekelezaji na sifa za miradi.
Wakili Ekuru Aukot, aliyeshiriki kuandaa Katiba ya 2010, alisema Ibara ya 6(2) inaeleza kuwa serikali za kitaifa na kaunti ni tofauti lakini zinategemeana, na zinapaswa kushirikiana kupitia mashauriano.
Mtaalamu wa utawala Peter Mbae alionya kuwa mashindano hayo yanatishia kudhoofisha ugatuzi na utawala bora.
Alisema miradi ya maendeleo ni ya wananchi, wala si viongozi wanaotaka kujipatia umaarufu wa kisiasa.
Wakili Steve Kabita pia alisema hakuna serikali inayopaswa kudai kumiliki au kujipa sifa za mradi uliotekelezwa na upande mwingine.
Mvutano huo umeenea hadi sekta ya barabara, ambapo magavana wanataka angalau asilimia 15 ya fedha za hazinaya ukarabati wa barabara, huku wengine wakitaka asilimia 42, zitengewe kaunti. Bunge la Kitaifa limependekeza asilimia tano pekee.
Magavana pia wamepinga utekelezaji wa mpango wa maeneo ya viwanda katika kaunti, wakisema baadhi ya miradi ilianzishwa bila mashauriano ya kutosha na kabla ya masuala ya umiliki wa ardhi kutatuliwa.
Wakati huo huo, serikali ya kitaifa imehusisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kukamilisha miradi iliyokwama, ikiwemo hospitali na viwanja vya michezo. Baadhi ya magavana wanahofia kuwa Rais atajipatia sifa za miradi hiyo baada ya kukamilika.
Hata hivyo, viongozi wanaounga mkono ushirikiano wanasema serikali zote mbili zina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alisema Katiba inazitaka serikali hizo kushirikiana kwa manufaa ya wananchi.
Mzozo huo unaendelea kuibua maswali kuhusu mipaka ya majukumu ya serikali hizo mbili, hasa pale miradi inapohusisha fedha za pamoja.
Huku nchi ikielekea uchaguzi mkuu wa 2027, wataalamu wanaonya kuwa ushindani wa kisiasa haupaswi kuchelewesha huduma wala kufuta mafanikio ya ugatuzi.