HabariHabari za Kitaifa

Bunge lakataa masharti magumu ya kuwaondoa wabunge madarakani

Na SAMWEL OWINO October 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

JARIBIO la baadhi ya wabunge kutaka masharti magumu ya kuwaondoa mamlakani wabunge kupitia kura ya wananchi limefeli Bungeni wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi wa 2024.

Mbunge wa Suba North Millie Odhiambo aliongoza juhudi za kutaka mbunge aondolewe mamlakani baada ya kupatikana na hatia ya kosa kubwa la jinai, kuhukumiwa na kufungwa jela kwa angalau miezi sita.

Alisema masharti yaliyopendekezwa na Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria yalikuwa rahisi mno na yanaweza kutumiwa vibaya kisiasa.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo, hatua ya kumuondoa mbunge  ingeanzishwa baada ya thuluthi moja ya wapiga kura waliosajiliwa katika kila wadi ya eneo bunge husika kutia saini ombi hilo. Kwa seneta, thuluthi moja ya wapiga kura katika kila eneo bunge la kaunti ingehitajika.

Hata hivyo, uchaguzi mdogo ungeamuliwa kwa kura nyingi zaidi, huku mchakato wa kumwuondoa mbunge ukiruhusiwa kuanzishwa baada ya miaka miwili tangu kuchaguliwa kwake.

“Hata kama nitasimama peke yangu, nitasimamia ukweli wangu. Ninapinga marekebisho haya kwa sababu kiwango mnachopendekeza ni cha chini mno,” alisema Bi Odhiambo.

Mbunge wa Saku, Dido Raso aliunga mkono msimamo huo, akionya kuwa kupata saini za thuluthi moja ya wapiga kura katika kila wadi kunaweza kuwa rahisi na kusababisha mchakato huo kutumiwa vibaya.

Lakini Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na mwenzake wa Wachache Junet Mohamed walipinga masharti magumu, wakisema wananchi hawapaswi kuzuiwa kutumia haki yao ya kuwaondoa viongozi wasiowaridhia.

Ichung’wah alisema kuweka kiwango cha asilimia 50 katika kila wadi kungeweza kurudia makosa yaliyofanya mahakama kufutilia mbali sheria za awali.

Ibara ya 104 ya Katiba, inaitaka Bunge kuweka sheria zinazoeleza sababu na utaratibu wa kuwaondoa wabunge madarakani.

Mnamo 2017, Mahakama Kuu ilitangaza vifungu kadhaa vya sheria kuhusu kuondolewa kwa wabunge kuwa kinyume cha Katiba, ikisema vilikuwa na dosari.

Mjadala huo unaendelea huku Bunge likijaribu kuweka mfumo wa kisheria utakaowezesha wananchi kuwawajibisha wawakilishi wao bila mchakato huo kutumiwa vibaya.