Habari Mseto

LAMU: KDF yatoa matibabu ya bure kwa wakazi 500

August 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI zaidi ya 500 kutoka Kotile na viungani mwake walipokea matibabu ya bure kutoka kwa maafisa wa jeshi (KDF) kama njia mojawapo ya kudumisha ushirikiano mwema kati ya raia na walinda usalama.

Wanajeshi hao ni miongoni mwa wale wanaoendeleza operesheni ya kiusalama inayolenga kuwasaka magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.

Kambi hiyo ya matibabu ya bure iliandaliwa katika kijijiji cha Kotile karibu na mpakani mwa kaunti za Garissa, Lamu na Tana River.

Wagonjwa wafurahia huduma za matibabu za maafisa wa KDF. Picha/ Kalume Kazungu

Waliofika kutibiwa walitoka vijiji vya Kotile, Hulugho, Ijara, Sangailu, Masalani, Hara, Korisa, Abartilo, Kitere, Mwena, Mnazini na Ngumu.

Wakazi wakiwemo wazee, akina mama wajawazito na watoto ambao wamekuwa wakihangaika kwa kukosa matibabu kwenye maeneo husika walipata fursa ya kutibiwa maradhi mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa matibabu ndani ya jeshi la Kenya (KDF).

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo iliyochukua siku nzima, daktari mkuu msimamizi katika jeshi, Kapteni Brian Ayacko alisema maradhi yaliyojitokeza kwa wingi miongoni mwa waliopokea tiba yalikuwa yale ya kuharisha, matatizo ya kifua hasa kupumua miongoni mwa watoto.

Mmoja wa maafisa wa KDF akipiga soga baadhi ya akina mama waliokuwa wakisubiri kutibiwa Kotile.

Maradhi ya kiakili miongoni mwa watoto na watu wazima pia yalijitokeza kwa wingi wakati wa kambi hiyo ya matibabu, jambo ambalo lilipelekea baadhi yao kupewa rufaa kutafuta tiba maalum kwenye hospitali ya rufaa mjini Garissa na sehemu zingine za Kenya.

“Tuko hapa Kotile leo kuwatibu wakazi. Hii ni mojawapo ya mikakati ya kudumisha uhusiano mwema kati ya KDF na wananchi. Nimetibu jumla ya watoto 99 wa  umri wa miaka mitano kwenda chini, 398 ambao wanazidisha miaka mitano, wanaume 195 na akina mama 203. Jumla ya waliotibiwa kwenye kambi ya leo hapa Kotile ni watu 497.

Maafisa wa KDF wakitibu wagonjwa eneo la Kotile, mpakani mwa kaunti za Garissa, Lamu na Tana River. Kambi hiyo ya matibabu iliweza kuhakikisha zaidi ya wakazi 500 wanapokea matibabu hayo ya bure. Picha/ Kalume Kazungu

Maradhi yaliyojitokeza kwa wingi ni kuharisha, shida ya kupumua na matatizo ya akili. Tutaendelea kushirikiana na wananchi ili kuandaa shughuli kama hizi maeneo mbalimbali ya Garissa, Lamu, Tana River na sehemu zingine za nchi,” akasema Bw Ayacko.

Shughuli hiyo ilishuhudia ulinzi mkali wa maafisa wa KDF ambao walishika doria kila mahali wakati matibabu yalipokuwa yakiendelea kwenye hospitali ndogo ya Kotile.

Mmoja wa wakazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hospitali ya Kotile, Abdi Ahmed Buro, aliitaja shughuli ya matibabu ya bure kutoka kwa KDF kuwa muhimu kwa wakazi ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta tiba eneo hilo.

Mmoja wa wazee wagonjwa afurahia huduma za maafisa wa KDF eneo la Kotile. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Buro alisema wakazi wamekuwa wakilazimika kutumia njia za kitamaduni, ikiwemo miti shamba ili kujitibu kwa kukosa huduma za afya eneo hilo.

“Tunawashukuru KDF kwa juhudi zao katika kuhakikisha wanapeleka huduma za matibabu eneo hili ambalo liko na changamoto tele za afya. Hospitali nyingi ziko maeneo ya mbali na pia huduma zinazotolewa ni za kiwango cha chini ikilinganishwa na matatizo ambayo wananchi wako nayo. Tutaendelea kushirikiana na KDF ili tupokee huduma zao za matibabu,” akasema Bw Buro.

Naye Bi Saharla Rabe Shurie, alisema akina mama wajawazito wamekuwa wakijifungulia chini ya miti kutokana na ukosefu wa huduma za afya eneo hilo.

Usalama ulivyoimarishwa Kotile wakati kambi ya matibabu kutoka kwa KDF ilipokuwa ikiendelea kwenye hospitali ya Kotile. Picha/ Kalume Kazungu

Aliwashukuru KDF kwa kuwaletea huduma za matibabu karibu nao.

“Akina mama wajawazito na watoto huwa hawapati huduma za kliniki hapa. Inakuwa vigumu kutokana na umbali uliopo kufikia huduma za afya. Wanawake wamekufa hapa wakati wakijifungua ilhali wengine wamelazimika kujifungua chini ya miti. Ningewaomba KDF na serikali kuendelea kusambaza huduma ya kambi za matibabu mara kwa mara,” akasema Bi Shurie.

Kwa upande wake, Mkuu wa KDF katika kambi ya Kotile, Meja Alfred Mwaro, aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kudumisha uhusiano mwema kati yao na walinda usalama.

Mmoja wa maafisa wa KDF akihutubia wanahabari. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema ushirikiano uliopo umechangia pakubwa kuleta utulivu na amani eneo hilo ambalo awali lilikuwa likishuhudia uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa magaidi wa Al-Shabaab.

“Wananchi wa hapa wamekuwa na ushirikiano mzuri na sisi. Operesheni yetu hapa imefaulu kupitia ushirikiano mwema uliopo. Mbali na kuwaletea matibabu ya bure, pia tumewachimbia visima vya maji.

Mwenyekiti wa Hospitali ya Kotile, Abdi Ahmed Buro. Aliwashukuru KDF kwa kuwaletea matibabu. Picha/ Kalume Kazungu

Pia tumekuwa tukiwapa chakula cha msaada. Ili kudumisha zaidi ushirikiano, huwa mara kwa mara tunaandaa mechi za mpira wa kandanda kati yetu na wanakijiji wa hapa,” akasema Meja Mwaro.