Habari za Kitaifa

Babu Owino aitwa kuhojiwa na DCI kuhusiana na madai ya uchochezi na ulanguzi wa pesa

Na BENSON MATHEKA July 23rd, 2024 1 min read

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameitwa kufika mbele ya wapelelezi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai  (DCI) kuhojiwa kuhusiana na madai ya uchochezi na ulanguzi wa fedha.

Kupitia barua, mbunge huyo aliagizwa kufika katika makao makuu ya DCI  kwenye barabara ya Kiambu jijini Nairobi Jumatano, Julai 24 saa 9 asubuhi.

Kulingana na maafisa hao wa upelelezi, Babu Owino aliitwa kutoa habari kuhusu madai ya kosa la uchochezi dhidi ya polisi na ulanguzi wa fedha.

“Ninakuomba, Babu Owino, uripoti kwangu katika kituo cha polisi katika makao makuu ya DCI, Kaunti ya Nairobi  Julai 24 saa tatu, mchana na uandikishe taarifa kamili kuhusu uchunguzi huo hiyo,” ilisoma sehemu ya ilani kutoka kwa Inspekta Mkuu Eunice Njeri.

“Ninaamini wewe, Babu Owino, unaweza kuwa ulihusika au una taarifa ambazo zinaweza kunisaidia katika uchunguzi wangu.”

Mbunge huyo alitahadharishwa kuhusu uwezekano wa kufunguliwa mashtaka iwapo atakosa kufuata agizo hilo na kujiwasilisha kuchunguzwa.

Kuitwa kwa Babu Owino na maafisa wa upelelezi wa DCI kunajiri huku akitoa msimamo mkali kupinga utawala wa Rais William Ruto.

Mnamo Jumatatu, akiwahutubia wakazi wa Kaunti ya Homa Bay, Owino alionyesha kuunga mkono vijana wanaoandamana.

“Kwa Gen Z wa nchi hii, tunajivunia nyinyi, tunapenda mnachofanya na tunajua tofauti kati ya Rais William Ruto na Gen Z,” Babu Owino alisema.