Dimba

Arsenal yajipata katika shida zile zile kwa misimu mitatu sasa; haiendi mbele, haisongi nyuma

Na MASHIRIKA, RUTH AREGE October 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, UINGEREZA

ARSENAL kwa mara nyingine tena imejipata katika njia panda katika mbio za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya mechi ya raundi ya tisa wikendi iliyomalizika.

Baada ya Liverppol kulazimisha sare ya 2-2 ugani Emirates Jumapili, Arsenal waliendelea kuganda nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 18 nao Liverpool walisalia nafasi ya pili na alama 22, alama moja nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City.

Katika misimu miwili iliyopita, vijana wa Mikel Arteta wamekuwa wakimaliza nafasi ya pili nyuma ya City na sasa wameachwa na mwanya wa alama tano.

Bukayo Saka alifungia Arsenal bao la ufunguzi dakika ya tisa kabla beki wa Liverpool Virgil Van Dijk kujibu dakika tisa baadaye. Mikel Merino alifungia Arsenal bao la pili dakika ya 43 kabla ya Mo Salah kuharibu hesabu za wenyeji kwa kufunga bao la kusawazisha dakika ya 81.

Gunners walipata pigo lingine kwenye mechi hiyo ambapo beki Gabriel Magalhães aliondoka uwanjani dakika ya 54 kutokana na jeraha la goti.

Arteta mara nyingi aliepuka kujibu maswali kuhusu habari za timu kabla ya mechi; kabla ya mechi hiyo ya kaskazini mwa London alinyamaza kuhusu jeraha la Saka ambaye wengi hawakutarajia kwamba angecheza.

Katika mechi nyingine, masaibu ya Erik ten Hag yaliendelea kuongezeka baada ya kipigo cha 2-1 dhidi ya West Ham katika uwanja wa London.

Jarrod Bowen alifunga penalti ya kutatanisha katika dakika za lala salama kipindi cha pili kuipa West Ham United ushindi wa 2-1 dhidi ya Manchester United.

Crysencio Summerville alifunga goli lake la kwanza akiwa ndani ya uzi wa West Ham dakika ya 74 naye Casemiro akasawazisha dakika ya 81 kabla ya Bowen kutupa kambani bao la ushindi.

West Ham walipanda hadi nafasi ya 13 kwenye jedwali wakiwa na pointi 11 baada ya mechi tisa, sawa na Manchester United wanaoshika nafasi ya 14.

Ingawa kipigo cha Man United kilikuwa mara yao ya pili tu katika mechi kumi katika mashindano yote, kitamuweka kocha Erik ten Hag katika presha tena kwani wameweza kushinda moja tu kati ya mechi zao nane zilizopita.

“Mara tatu msimu huu tumepitia hali ya kutokuwa na haki,” alisema Ten Hag. “Lazima tufunge goli, tumepata nafasi nyingi sana. Tunapaswa kuwa mbele kwa magoli mawili au matatu.

“Katika kipindi cha pili tulikuwa tukijaribu sana lakini tuliwaruhusu kuingia kwenye mchezo. Unapokuwa unashindwa 1-0 unapaswa kufanya mashmabulizi ya kutosha,” aliongezea.

“Hivyo kwanza kabisa, katika soka si kila wakati timu bora ndio inashinda, na leo dhahiri si jinsi VAR ilivyofanya kazi,” Ten Hag alisema.