Kimataifa

Gen Z Nigeria waanza maandamano ya siku 10 dhidi ya utawala wa Rais Tinubu


VIJANA wa  kizazi cha Gen Z nchini Nigeria wameanza rasmi maandamano yao ya siku 10 ya kupinga serikali ya Rais Bola Tinubu na kupanda kwa gharama maisha.

Maelfu ya vijana hao, jana Agosti 1, 2024,  walijitokeza katika majimbo na miji mingi nchini humo kuandamana kupinga utawala mbaya wa Rais Tinubu.

Vijana hao sasa wanaonekana kufuata nyayo za wenzao kutoka Kenya, Uganda na Bangladesh.

Vijana hao walikaidi agizo la Rais Tinubu la kuwataka wasitishe maandamano hayo huku akiwasihi wampe muda wa kufanya mageuzi katika serikali yake.

Baadhi ya maafisa wakuu katika serikali ya Tinubu walitaja maandamano hayo kuwa hayafai na kudai kuwa yamechochewa kisiasa.

Waandalizi wa maandamano hayo wanatoa wito kwa serikali itatue suala la ongezeko la bei ya mafuta, kurejeshwa kwa ushuru wa bei nafuu wa umeme, na kupunguzwa kwa ushuru wa uagizaji wa bidhaa miongoni mwa matakwa mengine.

Vikundi hivyo pia vinataka kubatilishwa kwa sheria ya kupandisha karo za elimu ya juu.

Pia wanadai uwazi na uwajibikaji katika utawala wa rais wao, ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa mishahara na marupurupu ya maafisa wa umma na kutengwa kwa hazina ya dharura ili kuwasaidia wafanyabishara ndogo ndogo.

“Tunaandamana kwa sababu tuna njaa,” mwanaharakati wa Nigeria Banwo Olagokun aliliambia shirika moja la habari.

Yeye ni sehemu ya Vuguvugu la Take It Back, mojawapo ya makundi ambayo yameitisha maandamano hayo ya siku 10.

“Tunaandamana kwa sababu bei za bidhaa zinaendelea kupanda jambo ambalo linatufanya tushindwe kujikimu kimaisha, Hatuwezi kununua vifaa kama vile chakula, maji, nguo na matibabu,” Bw Olagokun, aliongeza.

Nigeria inakabiliwa na suala la kupanda kwa gharama ya maisha.

Mfumuko wa bei wa kila mwaka ni asilimia 34.19, ambayo ni juu zaidi katika karibu miongo mitatu.

Bei za vyakula zimepanda kwa kasi zaidi – kwa mfano, bei ya viazi vikuu Lagos ni karibu mara nne zaidi ya bei ya bidhaa hiyo mwaka jana.