Habari Mseto

2007/8: Wengi waliolipwa fidia baada ya machafuko walikuwa wakora

December 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Joseph Openda

KIKUNDI cha wakimbizi wa ndani kwa ndani kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 kinaitaka mahakama kuishurutisha serikali kutumia orodha yao ya waathiriwa 96, 000 watakaolipwa fidia, kikisema wengi wa waliolipwa hawakufaa.

Wakati huohuo wizara ya usalama wa ndani inamulikwa baada yake kushindwa kuelezea namna ilitumia Sh6.5 bilioni ambazo zilipaswa kulipwa wakimbizi, katika sakata ambayo wakora wanadaiwa kumeza mamilioni ya pesa hizo.

Serikali ilishindwa kutoa sajili iliyotumika kuwalipa wakimbizi kortini, licha ya korti kutoa amri mara kadha kuwa ifanye hivyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Wakitumia wakili Wilfred Konosi, wakimbizi hao wanamtaka Jaji Joel Ngugi wa Mahakama Kuu ya Nakuru kuiamrisha serikali kutumia sajili yao kuwafidia watu walioadhiriwa na machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2007.

“Walalamishi wameruhusiwa kufanyia marekebisho kesi yao na kuweka maombi watakayotaka,” Jaji Ngugi aliamua jana.

Katika kesi hiyo waliyoshtaki mnamo 2016, waadhiriwa hao walishtaki katibu katika wizara ya usalama wa ndani, waziri wa ugatuzi na katibu katika wizara hiyo na Mwanasheria Mkuu.

Wanataka kupewa habari kuhusu namna na watu walionufaika na Sh6.5bilioni ambazo serikali ilitoa katika bajeti ya ziada ya 2016/2017 ili walipwe.

Waliilaumu serikali kwa kutekeleza shughuli ya kuwalipa waadhiriwa kwa njia haramu. Mwaka uliopita, wakimbizi hao walifanikiwa kuiomba korti kuamrisha serikali kusitisha malipo zaidi, hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa kikamilifu.