Habari MsetoKimataifa

Amerika si salama tena, ulimwengu waonywa

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

TAHADHARI ya usalama imetolewa kimataifa kwa watu wanaosafiri kwenda Amerika, kufuatia ongezeko la mashambulio ya bunduki nchini humo.

Mnamo Jumamosi, watu 20 waliuawa katika duka kuu lililo El Paso, Texas kisha wengine tisa wakauliwa kabla saa 13 kupita katika eneo la Dayton, Ohio.

Huku mataifa mengi yakiepuka kutoa tahadhari kwa raia wao, pengine kwa kuhofia kughadhabisha Amerika iliyo na ushawishi mkubwa ulimwenguni, Shirika la haki za kibinadamu la Amnesty International liliamua kujitwika jukumu hilo jana.

Wakati mwingi Amerika huwa haichelewi kutoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya mataifa mbalimbali hata kunapokuwa na maandamano ya umma lakini mataifa mengine huwa hayatoi tahadhari yoyote hata mikasa ya kutisha inapotokea katika taifa hilo linaloongozwa na Rais Donald Trump.

Kufikia jana, nchi mbili pekee ambazo ni Venezuela na Uruguay ndizo zilikuwa zimetahadharisha raia wao wawe waangalifu kama ni lazima wasafiri Amerika.

“Kuwa mwangalifu zaidi kila wakati na ujihadhari na watu wanaobeba bunduki. Epuka maeneo ambako watu wengi hukusanyika hasa hafla za kitamaduni, maeneo ya ibada, shule na majengo ya kibiashara. Kuwa mwangalifu zaidi unapoenda katika baa, vilabu na kasino,” ikasema taarifa ya shirika hilo ambalo makao yake makuu ya Afrika Mashariki yako Kenya.

Ripoti ya 2018 kutoka shirika la Bloomberg inaonyesha kuna Wakenya wasiopungua 120,000 ambao wanaishi Amerika kihalali.

Rais Trump amekuwa akilaumiwa kwa muda mrefu kutokana na jinsi alivyoshawishi serikali yake isipitishe sheria ambazo zingefanya iwe vigumu kwa raia kumiliki bunduki.

Kando na haya, kuna wanaolaumu utawala wake kwa kufanya chuki ikite mizizi zaidi miongoni mwa watu wa rangi tofauti, dini na misimamo mengine ya kijamii.

Amnesty ililaumu Serikali ya Trump kwa kushindwa kuweka mikakati ya kutosha kulinda usalama wa umma dhidi ya mashambulio kutoka kwa wenye bunduki.

“Kwa msingi wa sheria za kimataifa kuhusu haki za kibinadamu, Amerika ina jukumu la kupitisha mipango mbalimbali katika madaraja yote ya uongozi na kudhibiti umiliki wa bunduki ili kulinda haki za raia kuishi na kusafiri wakiwa huru bila tishio la mashambulio ya bunduki,” ikasema.