Baadhi ya wakazi washutumu hatua ya serikali kuufunga Mji wa Kale
Na MISHI GONGO
WAKAZI mjini Mombasa wameshutumu serikali kwa kufunga Mji wa Kale, wakiitaja hatua hiyo kuwa kandamizi na kwamba itasambaratisha biashara zao.
Wakazi katika mji wa Mombasa hutegemea Mji wa Kale kupata bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula na nguo.
Wakizungumza na Taifa Leo Alhamisi, baadhi ya wakazi hao wamesema wanahofia kupata hasara maradufu kupitia mpango huo.
Bi Munira Juma ambaye anafanya biashara ya chakula amesema kufugwa kwa eneo hilo kutamzuia kufanya biashara yake ambayo ndiyo inampatia kipato cha kila siku.
“Ninauza chakula eneo la Bondeni lakini tangu kuwekwa kwa marufuku ya sisi kutoka siwezi kufika eneo hilo; chakula hakiwezi kudumu kwa muda mrefu hivyo nahofia kupata hasara,” amesema.
Wengine wanaouza mavazi wamesema wanachuma zaidi msimu huu, hivyo kufungwa kwa eneo hilo kutaathiri biashara zao.
“Kumi la pili la Mwezi mtukufu wa Ramadhan na la tatu ndio wakati wetu wa kuchuma ambapo watu wengi hununua nguo nyakati hizi na sasa kukatazwa kwao kufika huku kutatuathiri pakubwa,” amesema Mohammad Ahmed muuzaji mabuibui eneo hilo.
Amesema japo kaunti imewaruhusu kutafuta maeneo mengine ya kufanya biashara zao, itakuwa vigumu kupata sehemu nyingine hasa katikati mwa jiji.
Wafanyabiashara hao ambao wengi wao wanahudumu katika soko la Marikiti wamesema kufungwa kwa soko hilo kutaathiri mji wa Mombasa kwa jumla kwani watu wengi hupata bidhaa zao katika soko hilo.
Vitu vinavyouzwa sana katika soko hilo ni mboga, nyama na nguo.
Jumatano, serikali ilitangaza kufungwa kwa Mji wa Kale Mombasa na Eastleigh jijini Nairobi ili kupunguza idadi ya maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema visa ya maambukizi katika maeneo hayo vilikuwa vinaongezeka kwa kasi mno hivyo serikali iliamua kufunga maeneo hayo ili kupunguza maambukizi au hata kuzima kabisa maambukizi.