Habari Mseto

Babu Owino asema mpango mzima ni kumng'oa Sonko 2022

June 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu kama Babu Owino, ametangaza nia yake kuwania ugavana wa Nairobi 2022.

Bw Owino ambaye wiki iliyopita alipata afueni wakati mahakama ya rufaa ilipothibitisha ushindi wake wa ubunge katika kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa mpinzani wake Francis Mureithi, alisema anaamini ana uwezo wa kutosha kutatua changamoto zinazokumba wakazi wa Nairobi.

“Nina hakika nitakuwa gavana kwa sababu najua historia yangu ya uongozi bora tangu nilipokuwa katika chuo kikuu. Katika eneobunge la Embakasi Mashariki, najua kile nimefanyia wakazi na najua nitakachofanyia wakazi wa nairobi,” akasema kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen jana, na kuongeza lengo lake kuu ni kuwa rais wa Kenya baadaye.

Kulingana naye, changamoto zilizo jijini kama vile uhaba wa maji, ukosefu wa ajira, barabara mbovu, takataka, miundomsingi duni ya elimu na uhaba wa masoko bora zinaweza kutatuliwa kirahisi kama kuna kiongozi aliyejitolea kikamilifu kutumia rasilimali zilizopo ipasavyo.

Hata hivyo, alijiepusha kukashifu utendakazi wa gavana wa sasa Mike Sonko akasema wakati wa siasa haujafika.

“Sasa ni wakati wa kuhudumia wananchi. Sonko alichaguliwa kuwa gavana na inahtajika apewe muda wa kuhudumia wakazi. Ikifika 2022 uamuzi utatolewa kama alifanya vyema,” akasema.

Mbunge huyo alidai kuwa kesi ya kupinga ushindi wake ilikuwa imechochewa kisiasa kwani hata wakati mahakama kuu ilipoagiza kura zihesabiwe upya ilibainika alikuwa mshindi ilhali ikaamuliwa kwamba hakushinda kihalali.