Baraka za 'Nabii' Owuor kwa wafanyabiashara Nakuru
PETER MBURU Na MAGDALENE WANJA
Wafanyabiashara mjini Nakuru wamekula vinono kwa kipindi cha siku nne, kufuatia uwepo wa ‘Nabii’ David Awuor aliyepelekea maelfu ya watu kutoka kona zote za nchi kufurika mji huo.
Uchunguzi wa Taifa Leo Jumamosi ulibaini kuwa mamia ya wafanyabiashara wamepiga kambi ndani na nje ya uwanja wa Nakuru ambapo mhubiri huyo alikuwa akiwapa chakula cha kiroho.
Uwepo wa maelfu hayo ya watu umepelekea kuwepo uzungukaji wa pesa kwa wingi sana ndani ya siku hizo.
Baadhi ya bidhaa zilizouzwa kwa wingi zaidi ni vinywaji kama maji, soda, chai na uji, vyakula vya aina zote, matunda na nyingine nyingi.
Wengi wa waliofanya biashara huko ni wageni ambao kwa kawaida hufanya biashara mahali kwingine, walimu waliofunga shule na wafanyakazi wengine wa maofisini walioamua kutumia fursa hiyo kupata hela.
“Siku za kawaida huwa nafanya biashara ya utingo katika matatu lakini tangu Alhamisi nimepiga kambi hapa kuuza vinywaji. Hadi sasa nimeuza gari moja na kila siku nimekuwa nikipata zaidi ya Sh5, 000,” akasema Bw Elijah Mwangi.
Bw Mwangi alieleza Taifa Leo kuwa hajalala tangu Alhamisi, kwani alikuwa akiuza kwa saa 24, kwa maelfu ya wateja hao.
Baadhi ya wakazi wa karibu na uwanja huo aidha waliamua kulia nafasi ya pekee kwa kukodisha vyumba vyao vya kulala kwa waumini waliofurika na kukosa pa kulala.
“Kwa siku tatu sijalala katika nyumba yangu nimekuwa nikikodisha watu watatu kila siku kwa Sh2,000 kila mmoja. Nimekuwa nikilala kwa rafiki yangu ili kupokea pesa hizo,” akasema Bw James Njenga kutoka mtaa wa London.
Wamiliki wa mahoteli nao walifurahia msimu huo wa mavuno tele, huku yakifurika na watu kila siku na mamia yaw engine kukosa nafasi.
“Wakati mwingine tumelazimika kuwaruhusu kulala wawili wawili katika chumba hata kama kwa kawaida huwa haturuhusu, ili wengine wasilale nje,” akasema mkurugenzi wa hoteli moja.