Habari Mseto

COVID-19: Mkenya afariki nchini Saudi Arabia

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MKENYA amefariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Saudi Arabia, kulingana na balozi wa Kenya nchini humo Peter Ogego.

“Balozi Ogego ametuarifu kuwa tulimpoteza Mkenya mmoja aliyeambukizwa virusi vya corona. Hiki ni kisa cha kwanza kuhusu Wakenya nchini Saudi Arabia,” Mohamed Weliye, Mkenya ambaye ni mshauri katika Mamlaka ya Masuala ya Kifedha, Saudi Arabia, akasema kupitia Twitter.

Awali, iliripotiwa kuwa balozi Ogego alitoa taarifa akiwashauri Wakenya nchini humo kuzingatia kanuni zilizowekwa na serikali hiyo kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Alisema ubalozi huo umesitisha shughuli zake za kawaida kwa muda usiojulikana. Wafanyakazi walihitajika kufanya kazi kupitia mtandao.

“Hii ni kulingana na juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona na kupunguza hatari ya wahudumu na wateja kuambukizwa,” akasema.

Kifo cha Mkenya nchini Saudi Arabia kinafikisha 10, idadi ya Wakenya ambao wamefariki katika mataifa ya kigeni kutokana na Covid-19.

Sita wamefariki nchini Amerika huku wawili wakifariki nchini Uingereza.

Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni Macharia Kamau wiki jana aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni kwamba Wakenya watano waliofariki Amerika walikuwa na matatizo mengine ya kiafya ambayo yalichangia vifo vyao baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

Hata hivyo, hamna Wakenya ambao wamefariki kutokana na Covid-19 nchini China ambako ndiko chimbuko la ugonjwa huo ambao tayari umewaua zaidi ya watu 200,000 kote duniani na 14 nchini Kenya.