Habari Mseto

COVID-19: Rais Kenyatta atia saini mswada wa kupunguza ushuru

April 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SASA ni rasmi kuwa waajiriwa wanaopokea mshahara usiozidi Sh24,000 kila mwezi hawatatozwa ushuru wowote na wale wengine wanaopokea mishahara ya juu watatozwa ushuru uliopunguzwa zaidi.

Na wafanyabiashara wadogo sasa watalipa ushuru wa asilimia moja kwa faida wanazopata kila mwezi badala ya asimilia tatu ambayo wamekuwa wakilipa tangu Januari 2020.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali za ushuru kuwa sheria.

Sheria hiyo ambayo pia imehalalisha pendekezo la Rais la kupunguza ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa bidhaa za kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14, inalenga kuwakinga Wakenya kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Wafanyakazi wanaopokea mishahara ya zaidi ya Sh24,000 kila mwezi pia watapata afueni kwani wamepunguziwa ushuru wa mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25.

Waajiri pia wamepunguziwa ushuru wanaolipa serikali kwa kiwango chicho hicho ili kuwapunguzia gharama wakati huu ambapo janga la corona limeathiri shughuli za kiuchumi.

Mswada huo ulipitishwa na wabunge mnamo Jumatano baada ya wao kuujadili hadi saa nne za usiku.

Mswada huo umewasilishwa kwa Rais Kenyatta mnamo Jumamosi katika Ikulu ya Nairobi na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.

Wengine waliokuwepo ni Kiongozi wa wengi Aden Duale, Waziri wa Fedha Ukur Yatani, Wakili wa Serikali Ken Ogeto, Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu Nzioka Waita, Naibu wake, Njee Muturi na Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai.