• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Familia yakabiliwa na mzigo wa kulipia upasuaji wa binti  yao

Familia yakabiliwa na mzigo wa kulipia upasuaji wa binti yao

Na PETER MBURU

Kwa Muhtasari:

  • Babake Jane Wacuka, aliamua kumgawia sehemu ya ini lake asimwone akiteseka tena
  • Familia hiyo masikini ilifanya mchango na kupata Sh3 milioni
  • Kadri anavyokua Wacuka, ini lake linazidi kuwa dogo

FAMILIA moja katika eneo la Bahati, Nakuru inatatizwa na mzigo wa kulea binti wa miaka 14, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa ini.
Ingawa mzazi wa mtoto huyo, Bw Geoffrey Warui aliamua kumgawia bintiye sehemu ya ini lake, shughuli hiyo inafaa kufanywa nchini India.

“Inaniuma sana kumwona mwanangu akiteseka kila wakati, amekuwa na matatizo mengi ya afya ambayo yameishia kuathiri elimu yake. Niliamua kumgawia sehemu ya ini langu nisimwone akiteseka tena,” Bw Warui akaeleza Taifa Jumapili.

Msichana Jane Wacuka, 14, amekuwa na ugonjwa wa ini (Liver Cirrhosis) tangu akiwa na miezi sita, jambo ambalo limetatiza hali ya maisha yake na elimu.
Leo, familia hiyo itakuwa ikifanya mchango nyumbani kwao eneo la Ndundori ili kujaza pesa zilizosalia.

Matibabu hayo ambayo yatahusisha upasuaji wa baba na bintiye kwa takriban saa 15, utafanyika katika hospitali moja nchini India na yatagharimu Sh7 milioni.

Familia hiyo masikini ilifanya mchango na kupata Sh3 milioni ambapo wazazi walizuru India mnamo Januari 14 pamoja na binti yao kwa ajili ya upasuaji, wakiwaacha marafiki na familia wakichangisha pesa zilizosalia.

“Utakuwa upasuaji wa wazi baina yangu na binti yangu tukiwa katika chumba kimoja na utaendeshwa na vikosi vitatu vya madaktari watano kila kimoja, kwa saa tano,” Bw Warui akaeleza.

Serikali ya kaunti ya Nakuru imekuwa ikishirikiana na familia hiyo kutoa msaada na iliahidi kuzidi kuwashika mkono.

“Tunaamini kuwa pesa zilizosalia zitapatikana ili mtoto huyo apone na erejelee maisha ya afya bora,” Spika wa kaunti Joel Kairu akasema.

Kulingana na babake mtoto huyo, kadri anavyokua Wacuka, ini lake linakuwa dogo na hivyo inakuwa vigumu kwa mwili wake kuendesha shughuli zake kikamilifu.

 

You can share this post!

Fujo chuoni baada ya mwanafunzi kuuawa

Atwoli ataka Duale apokonywe kazi

adminleo