Hatujatia chochote mdomoni tangu Jumapili, washukiwa wa ufisadi walia mahakamani
Na RICHARD MUNGUTI
MAWAKILI wa washukiwa 43 wa sakata ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) Jumanne walilalamika kuwa watazirai kortini kwa vile hawajapewa chakula tangu Jumapili usiku.
“Mara ya mwisho washukiwa hawa walipata chakula ni Jumapili usiku. Wamekuwa wakirudishwa gerezani nyakati za siku wakati chakula kimeisha,” walisema mawakili Kirathe Wandugi , Cliff Ombeta na Dunstan Omari.
Mawakili hao walisema washukiwa hufika gerezani wanakozuiliwa usiku wa manane na kupata chakula kimeisha.
Jumanne asubuhi walirauka alfajiri kufikishwa kortini kabla ya “ kufungua kinywa.”
“Washukiwa hawa hawaelewi kinachoendelea kwa sababu ya njaa. Washukiwa wanaugua na wanahitaji kunywa dawa. Naomba wakubaliwe kunywa maji na ikiwezekana wapewe biskuti,” alisema Wandugi.
“Ni kwa ajili ya washukiwa wote ama ni kwa wachache,” aliuliza hakimu mkuu Douglas Ogoti.
“Ni kwa wote,” mawakili wote 35 wanaowatetea washukiwa walijibu.
Ilibidi wakili Bw Wandugi aeleze hali ya washukiwa hao kesi ikiendelea mwendo wa saa saba kasorobo.
Bw Wandugi aliomba mahakama iamuru washukiwa hao wapewe maji na biskuti “wasizirai kwa sababu ya njaa na kiu.”
“Washukiwa hawa hawajakula tangu Jumapili usiku .Wanahisi njaa kali na baadhi yao wanamatatizo ya kiafya. Naomba mahakama iamuru wapewe maji tu wanywe kesi ikiendelea kwa vile wanaumia sana. Na hata ikiwezekana wapewe biskuti watulize makali ya njaa,” Bw Wandugi alimsihi hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti.
Kabla ya Bw Wandugi kufichua hali ya washtakiwa hao, washukiwa Bi Anne Wambere Ngirita na Lucy Ngirita walikuwa wamesema kuwa “wako karibu kuzirai kortini kwa vile hawajakula tangu Jumapili usiku.”
Washukiwa hao walielezea Taifa Leo kuwa, hajakula tangu Jumapili usiku na Jumatatu walipewa vitafunio na jamaa wao waliotembelea kortini kusikiza kesi dhidi yao.
“Nilipewa Samosa moja tu na chupa ndogo ya maji. Sijala tangu Jumapili usiku. Naumia. Hata simu sijakubaliwa kupiga. Nachukuliwa kama mfungwa ilhali nilifikishwa kortini wiki iliyopita,” alisema Bi Anne Wambere Ngirita.
Aliongeza kusema hata hajui hali ya mtoto wake kwa vile hajakubaliwa kuwasiliana na mlezi wake.
Bw Ogoti aliamuru washukiwa wakubaliwe kunywa maji. Walipewa peremende badala ya biskuti.