Hatutakubali Jumwa chamani, ajitetee debeni – ODM
Na SAMUEL BAYA
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimesisitiza kuwa hakitamkubali tena mbunge wa Malindi Aisha Jumwa kikisema kinajiandaa kwa uchaguzi mdogo eneo hilo.
Bi Jumwa alipata agizo kutoka kwa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa kusimamishwa kutimuliwa na chama hicho
Akiongea katika shule ya sekondari ya Palakumi eneo la Ganze, katibu mkuu wa chama hicho Bw Edwin Sifuna alisema kuwa uamuzi wa kumtimua Bi Jumwa hautabadilishwa kamwe.
“Mimi ni wakili na hata nilipokuwa nikifanya juhudi za kumfukuza Bi Jumwa chamani, nilitumia vigezo vyote vifaavyo. Kwa hivyo huyu mama haruki kamba. Tunarudi kwa uchaguzi mdogo hivi karibuni Malindi,” akasema Bw Sifuna.
Aidha katibu huyo alisema kuwa wakazi wa Kilifi walipigia kura nyingi chama cha ODM na akasema kuwa umaarufu wa chama hicho katika kaunti hiyo bado uko imara.
“Ninataka kutangaza leo hii nikiwa hapa Ganze, Kilifi kwamba kifo cha kisiasa cha Bi Jumwa kilitangazwa kitambo na baraza kuu la chama chetu.
Na sasa hata Bw Mtengo ungelikuwa tayari uko Malindi kuanza mikakati yako ya kutafuta kura maanake tunarudi kwa debe Malindi,” alisema Bw Sifuna.
Na katika kile ambacho kinaonekana kama kumlenga Gavana wa Kilifi Bw Amason Kingi, Bw Sifuna alisema kuwa yeye ataongoza chama kumfanyia kampeni mwaniaji wa ODM atakayeidhinishwa Malindi.
Mwezi uliopita, Gavana Kingi alisema kuwa hayuko tayari kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Malindi kwa sababu alifanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba Bi Jumwa hafukuzwi ndani ya chama.
Hata hivyo, Bw Sifuna alisema kwa sasa wako na chaguzi ndogo tatu nchini ambazo wanashughulikia.
“Tukimalizana na hizi chaguzi tatu ndogo ninaamini kwamba tutakuja Malindi pia. Wewe kama hutatusaidia katika kampeni utakaa kando sisi tuendee mbele.
Lakini ninajua siku moja utakuja chamani na utakumbana nami. Kisha nitakuuliza ni kwa nini hukushirikiana nasi,” akasema Bw Sifuna.
Mbunge wa Kilifi Kusini Bw Ken Chonga alisema kama wabunge wa ODM wanaounga mkono chama na wako tayari kushiriki katika uchaguzi mdogo.