IG asisitiza polisi wa Kenya wataenda nchini Haiti
SERIKALI imewahakikishia raia wa Haiti kwamba imejitolea kutuma polisi wa Kenya kudumisha amani katika nchi yao.
Inspekta Jenerali wa polisi, Japhet Koome ambaye alifanya mazungumzo na ujumbe wa polisi wa Haiti uliozuru makao makuu ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), jijini Nairobi, alionea fahari ushirikiano utakaosaidia kurejesha utawala wa sheria na utulivu nchini Haiti.
Akizungumza baada ya kukutana na ujumbe huo jana, Koome alisema Kenya imejitolea kutuma polisi Haiti.
“Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imejitolea kushirikiana katika juhudi hizi, kwa manufaa ya watu wa Haiti, hasa wanawake na watoto,” Bw Koome alisema.
Mwenzake wa nchi Haiti alimhakikishia kwamba Haiti itawapa polisi wa Kenya usaidizi wote unaohitajika ili kufanikiwa katika shughuli hiyo.
“Tunategemea msaada wenu kwa manufaa ya watu wa Haiti, hasa wanawake na watoto,” afisa wa Polisi wa Haiti Joachim Prohete alisema.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Manaibu Inspekta Mkuu wa Polisi Kenya, Douglas Kanja na Noor Gabow, ambaye ni Afisa Mkuu wa ujumbe wa Kenya nchini Haiti.