Habari Mseto

KEBS yatakiwa izingatie uwazi kwenye tenda ya usafirishaji mizigo bandarini

Na KEVIN CHERUIYOT March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) limetakiwa kuwa na uwazi linapotoa zabuni kwa kampuni ambazo zinahusika na usafirishaji mizigo bandarini.

Hii ni kwa mujibu tenda ambayo ilitangazwa mnamo Januari mwaka huu na ilivutia kampuni mbalimbali zilizojitokeza kuwahi zabuni hiyo.

Hata hivyo, duru kutoka kwa waliotuma maombi ya tenda hizo, zinasema kuwa baadhi ya kampuni ambazo zimeorodheshwa, zilikataliwa kwenye baadhi ya nchi.

Kampuni hizo zilikataliwa kutokana na jinsi zilivyoshughulikia vibaya bidhaa na kuvuruga sheria na mwongozo zinazodhibiti usafirishaji wa mizigo bandarini.

Stakabadhi ambazo Taifa Leo imeziona zinaonyesha kuwa mmoja wapo ya kampuni ambayo iliorodheshwa na ina mizizi yake China, ilikataliwa kwenye baadhi ya mataifa  kwa kuvuruga na kukiuka mwongozo na sheria za usafirishaji mizigo katika nchi hizo.

“Ukaguzi uliofanywa na mashirika ya kukadiria ubora wa bidhaa Misri na Saudi Arabia unaanika jinsi kampuni hiyo ilivyokiuka sheria katika kusafirisha mizigo na ubora wa mizigo yenyewe kuvurugwa,” stakabadhi hizo zikaonyesha.

Kebs imetakiwa kutathmini mchakato mzima wa utoaji tenda hasa ikimakinikia viwango vya kimataifa vya kampuni, wateja, ubora wa stakabadhi zilizowasilishwa na kutiliwa kwa masharti ya ukaguzi.

Kwa upande Kebs yenyewe imenukuliwa ikisema mchakato wa utathmini utazingatia mfumo, uwajibikaji na masharti mengine mengi ya kisheria yanayohitajika kabla ya zabuni hiyo kutolewa.